Mahakama kuu nchini Kenya
imesimamisha kwa muda matumizi ya baadhi ya vipengee vya sheria ya
usalama yenye utata iliopitishwa na bunge na kuidhinishwa na Rais Uhuru
Kenyatta.
Wanasiasa wa upinzani waliwasilisha kesi mahakamani kupinga uhalali wa sheria hiyo kikatiba, huku wakisema inahujumu haki ya raia wa Kenya.
Sheria hiyo iliidhinishwa majuma mawili yaliyopita bungeni huku wabunge wa upinzani na serikali wakikabiliana kwa makonde na mateke.
Serikali ya Kenya inasema kuwa sheria hiyo itasaidia kukabiliana na makundi ya kigaidi kama vile lile la Al-Shabab.
Lakini upinzani umeibua utata kuhusu baadhi ya vipengee, kama kile cha kuwazuilia washukiwa hadi mwaka mmoja bila ya kufunguliwa mashtaka wakisema kinahujumu uhuru wa raia.