Kampuni
ya mtandao wa Google imeomba radhi baada ya picha za waziri mkuu wa
India Narendra Modi kuonekana katika picha za watu kumi wahalifu.
''Tunaomba
radhi kwa kuchanganyikiwa na kutoelewana ambako kumesababishwa na picha
hizo'',taarifa iliotoka kwa kampuni hiyo ilisema.Picha za Modi zinaonekana unapowatafuta watu 10 wahalifu pamoja na magaidi,wauaji na madikteta.
Viongozi wengine wakuu wanaopatikana ni waziri mkuu wa Delhi Arvind Kejriwal,wakili Ram Jethmalani na mtoro Dawood Ibrahim pamoja na mwigizaji wa Bollywood Sanjay Dutt ambaye kwa sasa anahudumia kifungo kutokana na mlipuko mkubwa uliotokea mjini Mumbai mwaka 1993.
''Haya matokeo yanatushangaza na hayawakilishi maoni ya Google'',kampuni hiyo ilisema katika taarifa yake iliotolewa jumatano usiku.
Msamaha huo unajiri baada ya wanasiasa wengi wa India kuonyesha wasiwasi wao katika mitandao ya kijamii.