DK MAGUFULI:TZ KAMA ULAYA INAWEZEKANA.

By | 22:36



Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli akiwahutubia wananchi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Mnadani Sengerema, mkoani Mwanza jana. Picha na Adam Mzee wa CCM.   

By Salam Maige, Mwananchi
Sengerema. Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema Tanzania inaweza kuwa kama nchi za Ulaya iwapo tu wananchi wataridhia aongoze Serikali ya Awamu ya Tano.
Dk Magufuli alisema hayo jana wakati akihutubia wananchi kwenye Uwanja wa Mnadani, Sengerema mkoani hapa.
Dk Magufuli, ambaye alisema anagombea urais ili kuondoa umaskini kwa wote, aliahidi kutekeleza ahadi yake ya kufufua viwanda, hasa vya pamba, kuendeleza ujenzi wa barabara na kuongeza nafasi za ajira kwa vijana.
“Inawezekana Tanzania kuwa kama Ulaya,” alisema Dk Magufuli mbele ya maelfu ya watu waliofurika kwenye Uwanja wa Mnadani. “Nichagueni, nitahakikisha nafufua viwanda na vitajengwa vingine.
“Nataka pamba inayolimwa hapa iwe inauzwa hapahapa nchini, nguo tutatengeneza sisi wenyewe kwa kutumia viwanda vyetu.”
Pia alisema atajenga pia viwanda vingine kama vya kuchakata matunda ili kutengeneza juisi.
“Nawaambia ndugu zangu wa Sengerema, mimi ni mwenzenu nimefundisha shule ya sekondari ya hapa Sengerema. Sitawaangusha,” alisema mgombea huyo ambaye ni Waziri wa Ujenzi.
Alirejea kauli yake kuwa umasikini wa wengi unatokana na watu wachache kujilimbikizia mali kwa kujihusisha na rushwa na ufisadi.
Alisema maendeleo yaliyokuwepo zamani, hayafanani na ya leo, na kuwataka wananchi kuwabeza wanaosema serikali haijafanya kitu.
Alitoa mfano wa barabara zilizojengwa kuwa zimerahisisha usafiri kutoka mkoa mmoja hadi mwingine, tofauti na ilivyokuwa zamani.
“Mimi Magufuli ndiyo nitakuwa rais?” aliwauliza wananchi ambao nao waliitikia, “ndiyo”.
Diallo
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo alimwambia Dk Magufuli kuwa kuna kero kubwa kwa wafanyakazi na malalamiko ya wananchi kukosa huduma muhimu kama uhaba wa dawa hospitalini.
“Mheshimiwa mgombea urais, kuna tatizo la maji. Maji hayapatikani kwa wananchi. Kuna shida kubwa ya umeme pamoja na barabara, lakini najua kwa sasa kama ni gari limepata dereva,” alisema Diallo, ambaye amewahi kuwa Waziri wa Maliasi na Utalii wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Alimuomba aanze kushughulikia kero hizo mara baada ya kuchaguliwa ili wananchi wazidi kuwa na imani na CCM.
Mgombea ubunge Ngeleja
Pia mgombea ubunge wa Jimbo la Sengerema, William Ngeleja alimuomba Dk Magufuli kuhakikisha ahadi zilizotolewa na serikali zinatekelezwa ikiwamo ya kujenga barabara ya kiwango cha lami kutoka Kamanga hadi Sengerema na kuongeza kivuko kingine Ziwa Victoria kutoka Busisi hadi Kigongo.
Waziri huyo wa zamani wa Nishati na Madini alisema wananchi wa Kamanga na Sengerema wamekuwa wakisumbuka na barabara kwa muda mrefu na kwamba ikijengwa kwa kiwango cha lami itainua uchumi wa Sengerema.
Pia Ngeleja alimtajia kero nyingine kuwa ni kulemewa kwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema.
Alimwomba Akiingia Ikulu ahakikishe anaongeza ruzuku kwa hospitali hiyo ambayo inamilikiwa na Kanisa Katoliki.


Newer Post Older Post Home