KESI YA KUTAKA TAFSIRI MITA 200 VYA KURA YAPANGIWA MAJAJI WATATU.

By | 22:11

Rais Jakaya Kikwete.
Kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mgombea ubunge Viti Maalum kupitia Chadema, Ammy Kibatala, imepangiwa jopo la majaji watatu wa kuanza kuisikiliza kuanzia leo katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo namba 37 ya mwaka huu, mlalamikaji anaoiomba mahakama itoe tafsiri ya kifungu cha 104 kidogo cha (1) cha Sheria ya Uchaguzi kama kinazuia ama la wananchi kukaa umbali wa mita 200 baada ya kupiga kura katika vituo vyao.
Jopo hilo la majaji linaongozwa na Jaji Sakieti Kihiyo na wengine ni Lugano Mwandambo na Aloysius Mjujulizi na itaanza kusikilizwa leo saa 3: 00 asubuhi mahakamani hapo.
Mgombea huyo wa ubunge viti maalum Chadema Jimbo la Kilombero, mkoani wa Morogoro, alifungua kesi hiyo Ijumaa iliyopita chini ya hati ya kiapo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Kupitia hatia hiyo, mgombea huyo ambaye pia ni mpiga kura mwenye maslahi na uchaguzi mkuu ujao, ameomba mahakama kwa mujibu wa kifungu hicho sura ya 343 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 ifafanue kuhusu haki za wapiga kura.
Mlalamikaji anaitaka mahakama iseme na kutafsiri kifungu hicho kinamaanisha nini kuhusu haki hiyo kufuatia kauli iliyotolewa na Nec pamoja na Rais Jakaya Kikwete kwamba wananchi wakishapiga kura hawaruhusiwi kukaa eneo la vituo vya kupigia kura umbali wa mita 200.
Aidha, anaitaka mahakama itamke kama ni halali kwa Rais na Nec kuzuia wananchi kukaa kwa utulivu umbali huo ama la.
 “Tume itamke kwamba kauli ya kuzuia haki ya wananchi ni uvunjifu wa katiba ya nchi kwa Watanzania,” ilieleza sehemu ya hati hiyo.
CHANZO: NIPASHE
Newer Post Older Post Home