Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa (kushoto) akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula walipohudhuria mazishi ya Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Dk Emmanuel Makaidi yaliyofanyika Dar es Salaam jana. Wa pili kushoto ni Mgombea mwenza wa urais wa Chadema, Juma Duni Haji na kulia ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia. Picha na Anthony Siame
Dar es Salaam. Mgombea urais wa Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa jana aliongoza mamia ya wananchi katika mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti mwenza wa umoja huo, Dk Emmanuel Makaidi huku baadhi ya viongozi wenzake wakisisitiza kuibuka na ushindi katika Uchaguzi Mkuu jumapili ijayo.
Mbali viongozi hao wa Ukawa kutambia ushindi huo, walielezea kifo hicho kilivyoacha pengo lisiloweza kuzibika kirahisi katika umoja huo, kukemea baadhi ya wanasiasa kumsahau Mungu na kuombea vifo wenzao, waliofariki katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi huo wa rais, wabunge na madiwani chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Juzi Ukawa ilitangaza kusitisha kampeni zake kwa saa 24 ili kutoa heshima za mwisho kwa Dk Makaidi ambaye wakati wa uhai wake alikuwa mwenyekiti wa NLD na mgombea ubunge wa Jimbo la Masasi.
Makaidi aliyefariki dunia Oktoba 15 kwa shinikizo la damu mkoani Mtwara, mwili wake ulizikwa jana saa 9:30 alasiri katika makaburi ya Sinza, Dar es Salaam.
Jambo lisilotarajiwa lililoibuka katika mazishi hayo ni kitendo cha takribani wananchi 100 kumfuata Lowassa nyuma huku wakimshangilia na kuimba “rais, rais, rais,” wakati akiondoka katika makaburi hayo na kuwapa wakati mgumu polisi kuwazuia.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria mazishi hayo ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, mgombea mwenza wa urais wa Ukawa, Juma Duni Haji, Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula.
Profesa Baregu
Wakizungumza katika ibada ya mazishi iliyofanyika Viwanja vya Karimjee, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu, alisema kifo cha Dk Makaidi ni ishara kuwa Ukawa itaibuka na ushindi mnono katika uchaguzi huo unaotajwa kuwa na kila aina ya ushindani.
“Tulishirikiana na Dk Makaidi kwa kila hali na alikuwa miongoni mwa wajumbe wa Bunge la Katiba waliosusia vikao vyake baada ya maoni ya wananchi kutupwa. Kifo chake ni ishara ya ushindi,” alisema Profesa Baregu.
Freeman Mbowe
“Ametuachia pengo lakini pengo hili litaongoza chachu yetu ya kupigana zaidi ili tushinde uchaguzi huu. Tunataka kufanya hivyo ili huko alipo (Dk Makaidi) aone tunachokipigania tumekipata,” alisema Mbowe.
Alisema Ukawa kwa kiasi kikubwa ulikuwa ukihitaji msaada wa Dk Makaidi, lakini kutokana na kifo hicho hawana jinsi, “Amekufa wakati tukiikaribia ndoto ya taifa na yake (Dk Makaidi) ya kuleta mabadiliko... alifanya kazi kubwa ya kupigania mageuzi nchini hakika tutamkumbuka sana,” alisema na kuongeza:
“Dk Makaidi amekufa akiamini Tanzania bila CCM inawezekana. Ni mtu ambaye alipigania mabadiliko bila kujali udogo wa chama chake na hakikuwa kikipata ruzuku,” alisema.
Tozi Matwange
Naye Katibu Mkuu wa NLD, Tozi Matwange alisitisha kusoma wasifu wa marehemu huyo ili kutoa nafasi kwa Lowassa aliyechelewa kufika katika ibada hiyo kuketi. “Nilisimama kusoma wasifu huu ili kumpisha rais wa awamu ya tano aketi katika kiti,” alisisitiza.
James Mbatia
Kwa upande wake, Mbatia alikemea tabia ya wanasiasa kuombeana mabaya ikiwamo vifo, huku akimpongeza Mchungaji wa Kanisa la Evangelist & Missions Ministries, David David kwa kukemea tabia hiyo, akisema inatolewa na watu wasio na hofu ya Mungu.
“Tuko pamoja na familia ya Dk Makaidi na tutajitahidi kwa uwezo na juhudi zetu zote ambazo ametufundisha Lowassa kwani yeye (Lowassa) ametukanwa sana, lakini amekuwa kimya. Misiba ni yetu sote na huunganisha taifa,” alisema.
Msemaji wa familia
Msemaji wa familia ya Dk Makaidi, Oscar Makaidi alieleza jinsi mwenyekiti huyo wa NLD alivyokuwa akipata fedha na kuanza kujiuliza aitumie kukiendeleza chama au kuihudumia familia yake.
“Mliobaki NLD mnatakiwa kukiendeleza chama hiki, yeye katoka lakini nyinyi mpo. Hata Ukawa mnatakiwa kutambua kuwa aliyekufa ni Makaidi si NLD, shirikianeni na viongozi wengine wa chama hiki, lazima msonge mbele kumaliza kazi iliyobaki,” alisema na kushangiliwa na waombolezaji.
Mutungi, Mziray
Jaji Mutungi alieleza jinsi Dk Makaidi alivyokuwa kiongozi shupavu, mwanamageuzi na mwenyekiti wa kwanza wa Baraza la Vyama vya siasa, huku Mwenyekiti wa sasa wa baraza hilo, Peter-Kuga Mziray akisema kifo hicho ni pigo kwa Ukawa na wapenda mabadiliko nchini.
Celestine Mwesigwa
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Celestine Mwesigwa na mwakilishi wa klabu ya Simba, Daniel Kamuna ni baadhi ya viongozi waliotoa salamu zao za ramsirambi na kueleza jinsi marehemu alivyoshiriki kuinua michezo nchini.
Dk Makaidi ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Simba miaka ya 70, ameacha mjane, watoto 10, wajukuu wanane na vitukuu watatu.