MAGUFULI AIWEKA SAWA DAR.

By | 10:51



SIKU tatu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli ameunguruma Dar es Salaam na kutoa wosia kwa Watanzania kwamba wanatakiwa kupiga kura kwa umakini ili wamchague kiongozi mwenye maamuzi makini na si maamuzi magumu.
Aidha, amesema akiapishwa kuwa rais, atahakikisha anaupatia ufumbuzi mara moja mradi wa maji kutoka Mto Ruvu hadi jijini Dar es Salaam aliosema umekwama kutokana mtu mmoja kwenda mahakamani kuupinga na mahakama kushindwa kutoa uamuzi kwa miaka mingi sasa.
Amesema pia mara daraja la Kigamboni litakapozinduliwa wananchi wote wataruhusiwa kupita bure, isipokuwa wenye magari na vifaa vingine vya moto ndio watakaolipia ushuru wa kuvuka. Aliyasema hayo jana alipofanya ziara ya kampeni katika maeneo ya Kigamboni, Mbagala, Temeke, Ubungo na Biafra mkoani Dar es Salaam.
Kuhusu maamuzi makini badala ya maamuzi magumu, Dk Magufuli alisema kiongozi wa maamuzi makini ndiye anayetakiwa kwa Tanzania ya sasa, ambayo inahitaji kupiga hatua za maendeleo kwa kasi, lakini kwa umakini mkubwa ili kuzuia mianya ya ufisadi.
Alisema kiongozi mwenye maamuzi magumu hahitajiki, kwa vile anaweza kutumia uamuzi wake mgumu kuiba mali za wananchi, kuwanyanyasa wananchi na pengine hata kujinyonga na kuwasababishia wananchi na Taifa hasara kubwa.
“Nawahakikishia Watanzania mimi nitakuwa Rais wa Maamuzi Makini kwa maendeleo ya watu wote bila kubagua kama ni wa CCM, Chadema, CUF, Ukawa, dini, au kabila lolote. Mimi Magufuli kwangu itakuwa ni Kazi Tu”, alisema.
Kuhusu tatizo sugu la maji katika Jiji la Dar es Salaam, Dk Magufuli alisema suala hilo limekuwa sugu kutokana na kukwama kwa mradi wa maji, uliokusudia kutoa maji Mto Ruvu hadi jijini Dar es Salaam, kutokana na mtu mmoja kuuzuia kwa kufungua kesi mahakamani akipinga mradi kupitishwa kwenye eneo alilojenga nyumba.
Alisema kinachosikitisha ni kuona kuwa kwa miaka mingi sasa, kesi hiyo haijatolewa uamuzi na hivyo mradi huo kukwama, suala ambalo limewafanya wakazi wa Jiji kuendelea kupata shida kwa kunywa maji machafu na kupata magonjwa ya mlipuko.
“Nasema mimi Magufuli bado siku tano nakwenda kuwa Rais, suala hili nakwenda kulipatia ufumbuzi mara moja. Haiwezekani watu wenye uwezo wanywe maji ya chupa ya Kilimanjaro halafu watu wengine tena wengi wanywe maji machafu.
Nichagueni Magufuli nikomeshe uozo kama huu,” alisema Dk Magufuli. Kuhusu mradi wa ujenzi wa daraja la Kigamboni, mgombea huyo wa CCM alisema mara daraja hilo litakapozinduliwa, wananchi watakaokuwa wakipita katika daraja hilo kwa miguu hawatatozwa fedha zozote na badala yake wale watakaopita na magari, ndio watatakiwa kulipa fedha kidogo za kuvuka.
Alizungumzia pia kuhusu mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kwamba mradi huo utaanza kazi mapema mwezi ujao, baada ya kushindwa kuanza mwanzoni mwa mwezi huu kutokana na baadhi ya maandalizi kukwama, ingawa alisema tayari mambo yote yamekamilika ikiwa ni pamoja na kuwasili kwa mabasi 140.
Akizungumza kwenye mkutano wa Biafra jimboni Kinondoni, Dk Magufuli alieleza kufurahishwa na mapokezi katika Jiji la Dar es Salaam kutokana na Jiji kushamiri kwa bendera za CCM, Chadema na CUF, akisema hizo ni dalili kwamba atashinda uchaguzi huo kwa kishindo.
“Nimefurahishwa sana na mapokezi haya, maana kila mahali ni bendera tu tena nyingi ni mpya, zinaonesha watu wamekesha usiku kucha wakiweka bendera ili kumkaribisha Dk Magufuli Dar es Salaam, kwa kweli nimefarijika sana kwa sababu mimi ndiye nitakayekuwa Rais wa Awamu ya Tano na nitakuwa Rais wa Watanzania wote,” alisema Dk Magufuli.
Alirejea kuelezea kazi kubwa iliyofanywa na serikali katika awamu zote, huku akikumbushia historia na shida walizokuwa wakikumbana nazo wananchi kabla ya kujengwa kwa barabara mbalimbali za lami nchini.
Alieleza mipango mbalimbali iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete katika kujenga barabara nchi nzima, ikiwemo pia katika Jiji la Dar es Salaam lenye msongamano mkubwa wa magari na pia ujenzi wa barabara za juu, akizirejea zile za Ubungo na Tazara.
Dk Magufuli aliwaomba wakazi wa Dar es Salaam kuwachagua wagombea ubunge Dk Didas Massaburi wa Ubungo, Abbas Mtemvu wa Temeke, Dk Faustine Ndugulile wa Kigamboni, Issa Mangungu wa Mbagala, Idd Azzan wa Kinondoni na Mussa Azzan ‘Zungu’ wa Ilala ili ashirikiane nao kuharakisha maendeleo ya Dar es Salaam.
HABARI LEO.
Newer Post Older Post Home