MAMIA WAUPOKEA MWILI WA DK.KIGODA,KUAGWA LEO KARIMJEE.

By | 00:20


  Dk. Kigoda akiwa kwenye matibabu India, aliposikia ninakwenda jimboni kwake, alikuja mara moja, nikamkabidhi Ilani ya Chama na nikazungumza naye kuhusu namna ya kutatua changamoto za wafanyabiashara, baadaye akarudi tena nchini India kuendelea na matibabu.
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.
Viongozi mbalimbali waandamizi serikalini akiwamo mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, jana walikuwa ni miongoni mwa mamia ya waombolezaji waliojitokeza kuupokea mwili wa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
 
Mbali ya Dk. Magufuli, wengine ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,  Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck  Sadik, Mkuu wa Mkoa  wa Tanga, Mwantumu Mahiza na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Henry Shekifu.
 
Dk. Kigoda alifariki dunia Oktoba 12, mwaka huu katika Hospitali ya Apollo nchini India, alikokuwa amepelekwa kwa matibabu ya figo.
 
Mke wa marehemu pamoja na watoto wake, pia walikuwa ni miongoni mwa waliowasili na mwili huo kutoka India.
Baada ya kuupokea mwili huo, ulipelekwa moja kwa moja katika Hospitali Kuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo kwa hifadhi.
 
Akimzungumzia marehemu, Balozi Sefue alisema kifo cha Dk. Kigoda ni pigo kwa serikali na kimewashtua wengi, hivyo itamkumbuka kwa mchango alioutoa.
 
Kwa upande wake, Dk. Magufuli alikielezea kifo hicho kuwa  pigo kwa chama chake kwa kuwa alitoa mchango mkubwa.
 
“Dk. Kigoda akiwa kwenye matibabu India, aliposikia  ninakwenda jimboni kwake, alikuja mara moja, nikamkabidhi Ilani ya Chama na nikazungumza naye kuhusu namna ya kutatua changamoto za wafanyabiashara, baadaye akarudi tena nchini India kuendelea na matibabu,” alisema Dk. Magufuli.
 
Mwenyekiti wa CCM mkoani Tanga, Shekifu alisema CCM imepata pigo kubwa kwa kuondokewa na kiongozi huyo ambaye  mchango wake bado ulikuwa unahitajika.
 
“Ni pigo kubwa kwa sababu ametoa mchango mkubwa kwa Chama, katika jimbo lake na bado tulikuwa tunamtegemea katika jimbo hilo alilokuwa analitetea. Sisemi hatutapata mtu wa kuziba, lakini huyu alikuwa ni mzoefu tofauti ni kwamba huyo mwingine tutakayempata, lazima aanze kujifunza,” alisema Shekifu.
 
Kwa mujibu wa mwakilishi wa familia, Athumani Mdoe, mwili huo utaagwa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaamn leo na kusafirishwa kwenda mjini Handeni kwa maziko.
 
Dk. Kigoda ni waziri wa pili kufariki dunia katika kipindi hiki cha kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
 
 Waziri wa kwanza kufariki dunia katika kipindi hiki ni Celina Kombani, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Septemba 24 , mwaka huu.  Wagombea wengine wa ubunge waliofariki dunia kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi ni Mohamed Mtoi, Septemba 13, mwaka huu, ambaye alikuwa anagombea ubunge Jimbo la Lushoto kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mgombea ubunge Jimbo la Arusha Mjini kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Estomiah Millah, Oktoba 9, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE
Newer Post Older Post Home