Kocha wa Man United, Louis Van Gaal
London, England. Ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Everton umemfurahisha kocha wa Manchester United, Louis van Gaal akiueleza kuwa umemsaidia kuwaimarisha kiakili wachezaji wake, ambao kwa sasa wanajiamini.
Alieleza juzi kuwa ushindi huo ugenini, Goodison Park ni salamu kwa wapinzani wao, CSKA Moscow ya Russia kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Man United ilipata mabao ya kipindi cha kwanza kupitia kwao, Morgan Schneiderlin na Ander Herrera na mtoto wa zamani wa Everton, Wayne Rooney aliyemaliza kazi na kumfariji Van Gaal. Mechi hiyo ilichezwa huku Everton ikiomboleza msiba wa aliyekuwa kocha wake, Howard Kendall aliyefariki Jumamosi.
Kendall aliyekuwa na umri wa miaka 69 ni mmoja wa makocha walioipa mafanikio klabu hiyo, Everton miaka ya nyuma, kabla ya kizazi cha sasa cha wachezaji. Pia, Kendall alicheza kwa mafanikio kwenye klabu hiyo ya Goodison Park, akiipa ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza mwaka 1979 kabla ya mfumo wa Ligi Kuu kuasisiwa, pia alikuwa kocha kwa vipindi vitatu tofauti.
Aliipa ubingwa wa ligi mara mbili, 1985 na1987, Kombe la FA, 1984 na lile la Washindi Ulaya, 1985
Man United ilichapwa mabao 3-0 na Arsenal wiki mbili zilizopita, lakini Van Gaal alivutiwa na kurejea kiwango kwa wachezaji wake.
Rooney alifunga bao lake la pili la Ligi Kuu msimu huu ambao amekuwa akisumbuliwa na kuporomoka kwa kiwango chake.
“Ulikuwa ushindi mzuri kwenye mchezo tuliocheza vizuri, niliwaeleza wachezaji wangu wote kwamba najivuna kuwa nao kwa sababu wameonyesha kiwango kizuri,” alisema kocha huyo Mdachi ambaye anaiongoza timu yake kuikabili CSKA mjini Moscow.