SIMBA YANG'ARA,YANGA,AZAM PABICHI.

By | 22:32

Beki wa Azam Pascal Wawa (katikati) akimdhibiti
Beki wa Azam Pascal Wawa (katikati) akimdhibiti mshambuliaji wa Yanga ,Donald Ngoma wakati wa mchezo wa ligi kuu Bara uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa ,Dar es Salaam jana.Timu hizo zilitoka sare 1-1.Picha na Said Khamis 
By waandishi wetu
Dar/ Mikoani. Azam imeing’ang’ania Yanga kileleni mwa ligi baada ya kuilazimisha sare 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, huku Simba ikivunja mwiko Mbeya kwa kuinyuka Mbeya City 1-0 kwenye Uwanja wa Sokoine.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kubaki kileleni kwa tofauti ya mabao baada ya kufungana kwa pointi 16 na Azam, wakifuatiwa kwa karibu na Simba na Mtibwa Sugar zenye pointi 15 kila moja.
Dar es Salaam; Washambuliaji wa kimataifa wameendelea kuthibisha ubora wao msimu huu, baada ya Mzimbabwe Donald Ngoma aliifungia Yanga bao la kuongoza katika dakika 45, akiunganisha vizuri krosi ya Malimu Busungu, kabla ya Kipre Tchetche wa Ivory Coast kuisawazishia Azam pasi ya Farid Mussa katika dakika ya 81.
Mabao yote mawili ya jana yametokana na uzembe wa mabeki wa timu hizo, kwani bao la Ngoma ni wazi mabeki wa Azam wanapaswa kujilaumu kwani Mzimbabwe huyo alipokea krosi Busungu na kuituliza kifuani mpira huo ulidunda chini kabla ya kuuwahi na kuunganisha akiwa ndani ya eneo la 18 bila ya kubunguziwa.
Uzembe huo wa Azam ulijirudia kwa Yanga nao ambao liwaacha wachezaji wa Azam, John Bocco, Shomari Kapombe, Farid na Tchetche kupigiana pasi ndani ya eneo la penalti kabla ya mfungaji kuupiga shuti golini lililomshinda kipa Ally Mustafa na kujaa wavuni.
Ngoma sasa amefikisha mabao matano sawa na Hamisi Kiiza wa Simba, huku Tchetche akifikisha mabao manne na kumfikia Mrundi Amissi Tambwe, huku mfungaji bora wa msimu uliopita Simon Msuva akiwa amefunga bao moja tu hadi sasa.
Yanga itajilaumu yenyewe kushindwa kuondoka na pointi tatu baada ya kiungo wake wa kimataifa wa Zimbambwe, Thaban Kamusoke kukosa penalti iliyopanguliwa na kipa Aishi Manura.
Penalti hiyo ilipatikana kiutata katika dakika 87, baada ya kipa Manura kugongana na Msuva aliyekuwa akijaribu kuunganisha mpira wa juu na mwamuzi kuamua adhabu hiyo.
Hii ni mechi ya tatu mfululizo sasa Yanga na Azam zinashindwa kufungani ndani ya dakika tisini, katika robo fainali ya Kombe la Kagame zilimaliza suluhu na Azam kushinda kwa penalti, kabla ya Yanga kulipiza kisasi katika Ngao ya Jamii iliposhinda kwa penalti baada ya kumaliza kwa suluhu.
Simba yavunja mwiko Sokoine
Mbeya: Simba imeendelea kuvunja miikoa baada ya jana kuitandika Mbeya City kwa bao 1-0, lililofungwa na beki Juuko Murshid katika dakika ya pili mchezo huo akimalizia kona iliyopigwa na Mohamed Hussein na kumpita kipa Juma Kaseja kabla ya Mganda huyo kusukumia wavuni.
Kocha Dylan Kerr amefanikiwa kuvunja rekodi zote mbaya za Simba msimu huu baada ya kushinda kwenye Uwanja wa Mkwakwani na sasa Mbeya na kuthibisha kweli lango lake kuipa ubingwa klabu hiyo.
Katika mchezo huo Mbeya City iliyocheza mechi yake ya kwanza bila ya kocha wake Juma Mwambusi aliyejiunga na Yanga, ilijaribu kutulia na kutegeneza mashambulizi kadhaa langoni mwa Simba, lakini bahati haikuwa yao.
Kiungo Haruna Moshi ‘Boban’ alionyesha uwezo mzuri katikati ya uwanja akishirikiana na Steven Mazanda, Christian Sembuli na Joseph Mahundi na kuifanya Mbeya City kutawala mchezo, huku washambuliaji wao wakishindwa kutumia nafasi walizopata.
Simba wenyewe wakicheza kwa kujihami na kushambulia kwa kushtukiza wakiwatumia zaidi viungo watano Jonas Mkude, Said Ndemla na Mwinyi Kazimoto, Justine Majabvi na Abdi Banda kupitisha mipira mirefu kwa mshambuliaji wao Mussa Mgosi.
Tanga: Coastal Union imeshindwa kutumia uwanja wake wa nyumbani baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Shujaa wa Mtibwa katika mchezo huo alilikuwa ni Ali Shomari aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Hassan Mganga katika dakika 70 na kujihakikishia pointi tatu muhimu ugenini.
Katika michezo mingine, Mshambuliaji Elius Maguri alifunga mabao mawili na Pastory Atanas alifunga moja wakiiongoza Stand United kushinda 3-0 dhidi Prisons kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Nayo Ndanda ikiwa nyumbani imelazimishwa suluhu Toto Africans, huku Atupele Green akikosa penalti. Majimaji ilishinda 1-0 dhidi ya African sport, shukrani kwa bao la Hassan Hamis.
Imeandaliwa na Oliver Albert (Dar), Mwanahiba Richard (Mbeya), Burhani Yakubu (Tanga), Masoud Masasi (Shinyanga)

Newer Post Older Post Home