Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman.
Kikwete alisema azimio la tano la Bunge lilitaka aunde tume huru ya kijaji kuchunguza dhidi ya majaji waliotajwa kupata mgawo wa fedha zilizochotwa katika akaunti hiyo.
“Azimio hili nimelipokea na tumelijadili lakini itabidi izingatie utaratibu wa kisheria kushughulikia suala hili linatakiwa lianzie mahakani kwenyewe hili halianzii kwa Rais wala Bunge, ”alisema jana jijini Dar es Salaam wakati akilihutubia Taifa kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Rais Kikwete alisema kwa mujibu wa sheria, Tume ya Mahakama ndiyo inatakiwa ijadili suala hilo na itakapobaini kuna ukiukwaji wa maadili ndipo linapelekwa Rais kwa hatua zaidi kwa sababu yeye (Rais) ndiye anateua majaji hao.
Rais Kikwete alisema kuwa mchakato wa kuwachunguza majaji kabla ya kuwachukulia hatua unapaswa kuhusisha uundaji wa tume ambayo inajumuisha majaji watatu kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.
Alisema kwa sasa suala hilo amemuachia Jaji Mkuu alishughulikie kwa mujibu wa utaratibu wa kisheria na baada ya hapo ndipo litapelekwa kwake huku akisema lengo ni kuondoa mwingiliano wa mihimili.
Majaji hao ni Jaji Aloysius Mujulisi anayedaiwa kupokea mgawo wa Sh. milioni 40 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa VIP Engineering and Marketing Limited, James Rugemalira na Jaji John Ruhangisa aliyepokea Sh. milioni 400 kutoka kwa Rugemalira.
MMILIKI WA FEDHA ESCROW
Kuhusu umiliki wa fedha za Tegeta Escrow iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hazikuwa za umma kama ilivyoelezwa bungeni.
Alisema fedha zilizochukuliwa katika akaunti hiyo ni za kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ambayo ililipwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kama tozo ya kuliuzia umeme shirika hilo.
Aidha, alisema fedha zilizokuwamo katika akaunti hiyo ni Sh. bilioni 202.9 na siyo Sh. bilioni 306 kama ilivyoelezwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wakati ikiwasilisha ripoti yake kwenye mkutano wa 16 na 17 wa Bunge mwezi uliopita.
Alisema akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa maalum baada ya kutokea mgogoro kati ya IPTL na Tanesco, Tanesco ikilalamika kutozwa fedha nyingi na IPTL za tozo ya uwekezaji kuliko gharama za uwekezaji.
“Escrow ni akaunti maalum inayoanzishwa kwa sababu maalum kwa masharti maalum na kazi ikiisha hufungwa na akaunti hiyo husimamiwa na wakala ambaye ni Benki Kuu ya Tanzania, wakala huyo ndiye mwenye jukumu la kusimamia malipo wakati ukifika,” alisema Rais Kikwete.
Alisema fedha hizo zilikuwa zinahifadhiwa katika akaunti hiyo ili mgogoro kati ya Tanesco na IPTL utakapokwisha IPTL iweze kulipwa fedha zake kwa sababu zilitokana na kuiuzia Tanesco umeme.
“Kumekuwa na madai kwamba fedha hizi mwenyewe nani, je, ni IPTL au Tanesco, na kama ni za Tanesco maana yake ni za umma, lakini fedha hizi ni za IPTL kwani ndiyo mlipwaji ambaye alilipwa kutokana na tozo za kuuuza umeme Tanesco,” alisema.
Rais Kikwete alisema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti yake, alieleza kuwa fedha hizo zinaweza kuwa za umma au za IPTL, lakini wakati huo akawatahadharisha Tanesco waache kuhesabu fedha hizo zilizopo Escrow ni za kwao.
Kuhusu kodi, alisema katika kipindi cha miaka saba ya mgogoro kati ya Tanesco na IPTL, bahati mbaya Tanesco ilikuwa haijakokotoa kiwango ambacho ni cha kwake na ilipoamuliwa IPTL alipwe chake kodi ilikuwa haijakatwa.
“Ilipoamuliwa IPTL apewe chake maana ya pili ipo kodi ya serikali na kwa mujibu wa taarifa ya CAG iliyodhibitishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kodi ilikuwa haijalipwa zaidi ya Sh. bilioni 21.7,” alisema.
Rais Kikwete alisemaTRA imeshapeleka madai kwa kampuni ya PAP kuitaka ilipe kodi ya Sh. bilioni 21.7 na wahusika wamekubali kufanya hivyo.
AMPONGEZA GHASIA
Kuhusu uamuzi wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia, kuwafuta kazi wakurugenzi siata, watano kuteungua uteuzi wao na sita kuonywa kutokana na kuvuruga uchaguzi wa Serikali za Mitaa, alimpongeza kwa uamuzi huo na kwamba alipopelekewa taarifa alitoa baraka zake.
Alisema kila mtumishi wa umma atambue kuwa asipotimiza majukumu yake, kuna adhabu ataipata hasa ikizingatiwa kuwa watumishi hao hao ndio watakaosimamia uchaguzi mkuuwa mwaka 2015, hivyo adhabu hiyo litakuwa fundisho kwa wengine.
CHANZO:
NIPASHE