AMANI MIKONONI MWA VYOMBO VYA HABARI.

By | 21:59


Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kujiepusha kuandika habari zinazoweza kuhatarisha amani ya nchi huku vikitanguliza utaifa mbele badala ya maslahi binafsi, jambo litakalofanya utulivu kutawala katika uchaguzi mkuu.

Wito huo ulitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Selemani Mzee, wakati akifungua mdahalo wa wazi kuhusu amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika siku sita zijazo.

Mdahalo huu wa wazi wa amani wakati na baada ya uchaguzi, uliwashirikisha wananchi wa kawaida, wanasiasa, viongozi wa dini pamoja  na vyombo vya dola.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Kilolo, aliwataka wanasiasa kunadi sera zao bila kutumia lugha za uchochezi huku akiwataka viongozi wa dini kutotumia nyumba za ibada kufanya siasa.

Mzee alisema waandishi wa habari wanafanya kazi nzuri, lakini muhimu ni kulitanguliza taifa kwanza kwa kuandikwa na kutangaza habari zikiwa zimeweka utaifa mbele ili amani ya Tanzania iendelee kudumu.

Tuna uzoefu na mataifa mengine ambayo vyombo vya habari havikutumika vizuri na matokeo yake kukatokea vurugu na mauaji, alisema Mzee.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi, limesema halitasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na vurugu kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramandani Mungi, alisema endapo wakiwakamata wahalifu ambao wanataka kuvuruga amani kwenye mkoa wa Iringa, watashughulikiwa ipasavyo na kwamba jeshi hilo limejipanga kwa ajili ya kuwashughulikia watu ambao watavunja amani hususan kipindi hiki cha uchaguzi.

Kwa upande wake Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Iringa, Wilfred Myuyu, alisema maandalizi yanaendelea vema na Nec imewasilisha vifaa vyote vya kupigia kura kwa wananchi zaidi ya laki tano waliojiandikisha mkoani hapa.

Myuyu alisema Mkoa wa Iringa ulikuwa na mahitaji ya masanduku 4,923,  lakini waliyonayo kwa sasa ni 5,665 ambayo yapo tayari kwa ajili ya kusambazwa kwa kazi ya kupigia kura.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Newer Post Older Post Home