Akisoma tamko hilo jana jijini Dar es Salaam mbele ya wawakilishi wa asasi za kiraia 300 nchini, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, alisema kuna vitisho vimeanza kutolewa na kuonesha vyombo hivyo siyo msaada kwa wananchi bali vinatumika.
“Majeshi kwa Bara na Zanzibar, yamekuwa yakifanya mazoezi waziwazi na karibu na makazi ya watu hali inayosababisha uoga na hofu kwa wananchi.
Baadhi wameonekana wakitapakaa kwenye makazi ya wananchi huku wakiwa wamevaa sare zao,” alisema na kuongeza:“Vyomba hivi kwa namna yoyote visiegemee upande wowote wa chama cha siasa, bali vitende haki kwa vyama vyote na wananchi wote wakiwamo wagombea na wasikubali kuyumbishwa na mamlaka yoyote nje ya sheria.”
Naye Mratibu wa Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), zinaonyesha udhaifu mkubwa katika utoaji wa taarifa za msingi kwa wadau na umma kwa ujumla, mojawapo ikiwa ni idadi halisi ya wapigakura na vituo vya kupigia kura.
“Nec na Zec zitimize majukumu yao kisheria kwa kutangaza rasmi takwimu za mwisho za wapigakura na kujibu hoja zinazoibuliwa na wanasiasa badala ya kuwabeza na kuwapuuza..., itoe Daftari la Wapigakura lenye vigezo vyote kwa wadau na wananchi wote ili wapate fursa ya kurekebisha kasoro,” alisema.
Olengurumwa alisema, pia Nec ibandike majina ya wapigakura kwenye vituo vyote wiki moja kabla ya kupiga kura, ifanye kazi kwa uhuru, kufuata sheria, kusimamia kanuni wanazokubaliana na vyama vya siasa ikiwamo kujiepusha kukipendelea chama chochote wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.
Mtaribu huyo aliitaka Nec kutumia busara katika suala la kusuburi matokeo mita 200 kwa kuangalia hasara na faida za kuzuia wananchi kubaki vituoni kwa mujibu wa sheria, watoe maelekezo yenye kuzingatia maslahi ya taifa kwa wananchi badala ya kusikiliza upande wowote wa wanaovutana katika suala hilo.
“Mahakama isaidie kutatua mgogoro huu wa tafsiri ya kisheria ili kuepusha machafuko katika taifa, yanayoweza kutokea kutokana na imani kuwa kukatazwa kubaki vituoni kuna nia ya kutaka kufanya ujanja fulani kuhusu kura zao ikiwamo kuziiba,” alisema.
Katibu wa Baraza la Asasi za Kiraia, Ismail Suleiman, alisema wameitaka Nec na Zec kuwasaidia watumishi waliohamishwa kikazi tofauti na maeneo waliyojiandikishia na wanafunzi wa vyuo vikuu ili wapige kura ya rais ikiwa ni pamoja na kuwezesha teknolojia ya habari kuwezesha upigaji kura kuwa wa waliojiandikishia popote nchini bila matatizo yoyote kwa mfumo wa kielektroniki.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI