JK:MIAKA 10 YA URAIS INATOSHA KUFANYA MAMBO MENGI.

By | 23:24


Rais Jakaya Kikwete.
Rais Jakaya Kikwete (pichani), amesema kuwa miaka 10 ya uongozi inatosha kabisa kwa Mkuu wa Nchi kufanya mambo mengi na kwamba hahitaji muda zaidi kumaliza ajenda yake.
 
Aidha, Rais Kikwete amewataka watumishi wa Ikulu kumsaidia Rais ajaye kwa ari na nguvu zaidi kuliko hata walimvyosaidia yeye katika miaka yote 10 ya uongozi wake.
 
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipozungumza na watumishi wa Ikulu katika hafla ya chakula cha jioni.
Watumishi hao waliagana na Rais Kikwete waliyemtumikia kwa vipindi tofauti.
 
Akizungumza na watumishi hao, Rais Kikwete alisema  anaondoka madarakani kwa furaha hata kama anaona huzuni kuagana nao ambao amekaa nao kwa miaka mingi baadhi yao kwa miaka 10.
 
“Kwa hakika, naondoka mwenye furaha sana. Ni kweli nasikitika kuwa tunaachana, lakini mambo yote mazuri yana mwisho wake. Nimeifanya kazi ya urais kwa miaka 10, nyie mnajua aina ya kazi hii. Miaka 10 ni mingi. Ni miaka inayotosha kabisa kwa mkuu wa nchi kukamilisha ajenda yake. Sidhani kama mtu anahitaji zaidi ya miaka 10 kutekeleza ajenda yake ya msingi,” alisema na kuongeza:
 
“Na hata ukitaka kukaa zaidi, huwezi kuyamaliza yote. Mzee Nyerere alikaa miaka 23, hakumaliza yote na yaliyobakia alimwachia Mzee Mwinyi ambaye naye alimwachia yaliyobakia Mzee Mkapa. Rais Mkapa naye alifanya mengi, lakini hakumaliza yote na akaniachia mimi. Na mimi nitamwachia yaliyobakia Rais ajaye.”
 
Kuhusu Rais ajaye ambaye atakuwa mkazi mpya ndani ya Ikulu, Rais Kikwete alisema: 
“Napenda kuwaombeni msaidieni sana Rais wetu ajaye. Kwa hakika nawaombeni tumsaidie kwa ari na nguvu zaidi kuliko hata mlivyonisaidia mimi.”
 
CHANZO: NIPASHE
Newer Post Older Post Home