CHADEMA YAMSHTAKI KIKWETE UN.

By | 23:33


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema tayari kimeandika barua kwenda kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon, kumshtaki Rais Jakaya Kikwete.
 
Mwanasheria wa Chadema, John Mallya, aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa barua hiyo waliituma UN jana.
 
Mallya alisema lengo la barua ni kumshtaki Rais Kikwete kwa mataifa mengine kutokana na kauli yake ya kuwatisha Watanzania  aliyodai aliitoa Oktoba 14, mwaka huu ya kuwataka wapigakura kuondoka kituoni baada ya kupiga kura na endapo watakiuka watashughulikiwa.
 
Mallya alisema kauli ya Rais Kikwete ni kinyume cha Sheria ya Uchaguzi inayomtaka mpigakura kukaa mita 200 kutoka kituo cha kupigia kura.
 
“Kwa sababu Rais Kikwete hatuwezi kumshtaki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, ziko mamlaka ambazo tunatumia kumshtaki kama tulivyofanya kuiandikia barua UN na kupeleka nakala Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika, Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai na kusainiwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari,” alisema Mallya.
 
Kuhusu wananchi kukaa mita 200, Mwanasheria huyo wa Chadema alisema jambo hilo ni kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 1985 kifungu cha 104 inayomruhusu mpigakura kukaa nje ya mita hizo.
 
“Mwananchi haruhusiwi kukaa maeneo hayo akiwa na sare, nembo za vyama au kufanya alama zozote za kuashiria kampeni, lakini ukiwa nje ya mita hizo 200, unaweza kufanya jambo lolote hata kampeni,” alisema Mallya.
 
Akizungumzia suala la kuhamasisha amani wakati huu wa kuelekea kupiga kura na kutangazwa kwa matokeo, Mallya alisema chama hicho kinahubiri amani, lakini hakiwezi kukaa kimya endapo kutakuwapo uvunjifu wa sheria.
 
“Serikali na Tume, ifuate sheria kwa kuwapa wananchi wake haki ya kupiga kura na kulinda kura zao. Chadema kinahubiri amani na kinalinda amani, lakini hatutakaa kimya kama sheria zitavunjwa,” alisisitiza.
CHANZO: NIPASHE
Newer Post Older Post Home