Rais wa Uchina Xi Jinping amelihutubia bunge la Uingereza baada ya kupokewa kwa shangwe na taadhima na Malkia Elizabeth wa Uingereza.
Rais Xi yuko mjini London kwa ziara ya siku nne.
Maelfu ya raia wa China walipiga foleni barabarani kumpokea na walimpungia mkono alipoabiri kigari cha mwenyeji wake Malkia Elizabeth kinachovutwa na farasi kuelekea kasri la Buckingham.
Hata hivyo kumekuwa na maandamano kuhusu ukiukwaji wa haki za kibinadamu nchini china.
Vilevile kulikuwa na maandamano yaliyofanywa na wachina wanaomuunga mkono rais huyo na walikuwa wakipeperusha bendera nyekundu za China.
Inaaminika kuwa Malkia Elizabeth alimkabithi rais Xi mkusanyiko wa vitabu vilivyoandikwa na mwandishi maarufu Shakespear.
Aidha mke wake rais Xi , Peng Liyuan alitunukiwa mkusanyiko wa nyimbo za kitamaduni za kiingereza.
Bendi ya jeshi ilicheza muziki kuashiria mwanzo wa sherehe za kumkaribisha rais huyo kwenye eneo maalum ambapo askari walitumia farasi.
Malkia Elizabeth pamoja na mmewe Prince Philip walimkaribisha rais Xi Jinping na kama sehemu ya makaribisho kabambe milio ya mizinga 41 ilitikisa jengo la mnara mkuu wa London na katika medani ya Green Park jijini London.
Serikali ya Uingereza inalenga kupata angalau mikataba ya kiuchumi yenye thamani ya dola bilioni 50.