Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
Vwawa. Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amewataka wafuasi wa Ukawa wamchague kwa kura nyingi mgombea urais kupitia chama hicho, Dk John Magufuli ili waweze kufaidi mabadiliko ya kweli.
Kinana alisema hayo jana alipohutubia mkutano wa kampeni kumnadi mgombea huyo wa urais, wabunge na madiwani wa CCM uliofanyika mjini hapa.
Alisema pamoja na sheria za nchi kuruhusu vyama vingi, lakini mwaka huu kambi ya upinzani haina mgombea mzuri ikilinganishwa na yule wa CCM.
Kinana aliwaambia watu waliohudhuria mkutano huo kuwa si dhambi mashabiki wa Ukawa wote nchini wakamchagua kiongozi wa nchi anayefaa kwa utendaji na ukweli.
Alisema wafuasi wa Chadema miaka tisa iliyopita walikuwa na kampeni ya kupinga ufisadi, lakini hivi sasa wameiacha ili wasimchafue mgombea wao.
Kinana alisema kampeni ya ufisadi ilitumika kuipa nguvu Chadema.
Katibu mkuu huyo wa CCM aliwataka wafuasi wa umoja huo wa Katiba watafakari kwa kina sifa za wagombea wote kabla ya kupiga kura ikiwa ni pamoja na kuwapima kwa uadilifu wao mbele za jamii.
Wiki iliyopita, Kinana alianza ziara mikoani kuwanadi wagombea wa chama hicho itakayomfikisha katika majimbo 64 ya uchaguzi. Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utafanyika Oktoba 25.
MWANANCHI.