Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli akihutubia mkutano wa kampeni kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja Unguja, jana. Picha na Salim Shao
Zanzibar. Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli amesema atapambana na maharamia wa kigeni wanaovua samaki katika Bahari ya Hindi, ili kulinda uchumi wa Tanzania.
Akihutubia mamia ya wafuasi wa chama hicho katika uwanja wa Mnazi Mmoja katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Dk Magufuli alisema akiapishwa kuwa rais maharamia hao wakae chonjo kwa kuwa anazo mbinu zote za kuwashughulikia.
Dk Magufuli alisema maharamia wana meli kubwa za kisasa ambazo zinavua samaki usiku na mchana kwenye bahari ya Tanzania.
“Haiwezekani rasilimali ya nchi ziwe zinaibwa na viongozi tupo hatuchukui hatua nitayashughulikia maharamia yanayomaliza samaki wetu,” alisema.
Alisema baada ya kuzuia uharamia, atahamasisha wawekezaji kujenga viwanda vya kusindika samaki ili Watanzania waweze kupata ajira, kuchangia katika pato la Taifa kwa kodi na kutoa ajira kwa wananchi.
Alisema badhi ya maeneo ambayo yanafaa kwa viwanda vya kusindika samaki ni Dar es Salaam, Unguja na Pemba kwa sababu yamepakana na bahari.
Kuhusu muungano, Dk Magufuli alisema ataulinda kwa nguvu zote kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema akiingia madarakani atamaliza kero ndogondogo za muungano kwa kufanya vikao kati ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu alikuwa kwenye wizara inayojihusisha na muungano alianza kuzishughulikia, sasa naahidi kuwa tutazimaliza,” alisema.
Aliwaomba Wazanzibari `kumtosa’ mgombea wa urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia tiketi ya CUF, Maalim Seif Shariff Hamad kwa kuwa amekuwa akipinga hadharani mafanikio yaliyopatikana wakati naye ni makamu wa kwanza wa rais.
“Nakuhurumia sana Dk Shein umefanya kazi ngumu unaleta maendeleo kwa wananchi makamu wako anasimama hadharani anasema serikali haijafanya chochote, wananchi mtoseni huyo,” alisema.
Kwa upande wake, mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia chama hicho, Dk Ali Mohamed Shein alisema ole wao wanaopanga kufanya vurugu katika siku ya uchaguzi kwani atawashughulikiwa kikamilifu.
“Mimi bado ni Rais wa Zanzibar wanaopanga kufanya vurugu waache wajue Serikali ipo na mimi ndiye rais wake,” alisema.
Alisema Serikali haijalala inalinda amani na utulivu, wananchi wajitoke kupiga kura kwani kutakuwa na usalama wa kutosha.
Akimnadi Dk Magufuli, Dk Shein alisema ni lazima atakuwa rais wa awamu ya tano na wagombea wengine wanamsindikiza.
“Hata kwenye mbio kuna wasindikizaji inaonekana dhahiri kuwa wanamsindikiza Magufuli kutokana na rekodi zao kuwa mbaya,” alisema.
Alisema Magufuli ndiye kiongozi anayefaa kuwa amiri jeshi mkuu ambaye ana uwezo wa kuifanya kazi hiyo.
Naye Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alisema mgombea urais CUF, Maalim Seif aache visingizio vya kusema kuwa ataibiwa kura.
Alisema amekuwa akisingizia kuibiwa kura kwa miaka mingi sasa jambo ambalo halifai.
Alisema wafuasi wa CUF wamekuwa wakichana mabango na kuweka alama za X kwenye picha za Dk Shein katika maeneo ya Malindi na Chukwani.
Alisema kitendo hicho ni cha vurugu lakini Maalim Seif hawakemei wafuasi wake. ila yeye amekuwa akikemea CCM kuwa wanaleta vurugu.
“Tunaomba awakemee wafuasi wake waachane na vitendo hivyo,” alisema.
Kwa upande wake, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi aliwataka Wazanzibari wenye kuchagua wagombea wa CCM kwa kuwa chama hicho bado hakina mbadala.
“Tutafanya kila liwezekanalo kushinda uchaguzi huu kwa sababu tuna sifa ya kushika dola na tunastahili,” alisema.