Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka.
Hatua hiyo dhidi ya Prof. Tibaijuka ilitangazwa na Rais Kikwete jana zikiwa zimepita siku tano tangu waziri huyo atamke hadharani kwamba, kamwe hawezi kung'oka katika nafasi yake.
Prof. Tibaijuka alitamka hayo akipinga kuhusishwa katika kashfa ya kupokea Sh. bilioni 1.6 kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira, katika mazingira ya kutatanisha.
Rais Kikwete, ambaye alikuwa akizunguzumza na wazee wa Dar es Salaam jana, alisema amechukua hatua hiyo, baada ya kutafakari na kujiridhisha kuwa kitendo cha Prof. Tibaijuka kupokea fedha hizo alizodai kuwa ni za msaada wa moja ya shule zake na kuziweka kwenye akaunti yake binafsi, kuna msingu mkubwa kimaadili una upungufu.
Alisema kabla ya kuchukua hatua hiyo, walikaa na Prof. Tibaijuka na kuzungumza naye kuhusiana na kitendo hicho.
Rais Kikwete wakati akianza kuelezea jambo hilo jana, ghafla alipatwa na kikohozi hali iliyowafanya wazee pamoja na watu wengine waliokuwa wamefurika katika mkutano huo, kuanza kushangilia na hivyo kumfanya asite kuendelea kuzungumza kwa takriban dakika moja.
"Nimepata kikozi sijui ni kwanini?," alisema Rais Kikwete na kuzua kicheko kutoka kwa wazee na watu waliohudhuria mkutano huo.
Baadaye, Rais Kikwete aliendelea kusema kuwa mbali na kuzungumza na Prof. Tibaijuka, Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma nayo pia inaendelea kumhoji.
Alisema mazungumzo kati yake na Prof. Tibaijuka yalitaka kujua fedha hizo ni za nini, alizipata wapi na alizipataje.
Rais Kikwete alisema katika majibu yake, Prof. Tibaijuka alijitetea kuwa fedha hizo alipewa kwa ajili ya kushughulikia shule.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema pamoja na utetezi huo wa Prof. Tibaijuka, mambo makubwa yaliyotia shaka, ni pamoja na kama fedha hizo ni za shule, kwanini hazikwenda moja kwa moja shule, badala yake zikatumwa kwa jina lake?
Alisema katika utetezi wake kuhusiana na swali hilo, Prof. Tibaijuka alijibu kuwa ndiyo masharti aliyopewa na aliyetoa fedha hizo.
"Kwa hiyo, tumelitafakari sana. Katika kupokea fedha hizo na kuziweka kwenye akaunti yake, kuna msingi mkubwa wa kimaadili una upungufu," alisema Rais Kikwete.
Aliongeza: "Tumezungumza naye waziri huyu, tumemuomba atupe nafasi tumteue mwingine."
Kauli hiyo iliufanya ukumbi mzima wa mkutano kulipuka kwa mashingilio na kuimba CCM, CCM, CCM, kabla ya Rais Kikwete kuwaomba wazee na watu wengine waliohudhuria watulie ili wamalize mkutano.
Kuhusu Prof. Muhongo, Rais Kikwete alisema amemuweka kiporo kwa kuwa kuna uchunguzi ambao ameagiza ufanyike, kabla ya hatua stahiki kuchukuliwa dhidi yake.
"Sijapata majibu, siku zijazo yakija tufanye maamuzi,"alisema Rais Kikwete.
Alisema uchunguzi huo unafanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Jeshi la Polisi na tume hiyo, ikiwa ni utekelezaji wa azimio la saba kati ya nane yaliyopitishwa na Bunge kufuatia uchotwaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Maazimio hayo, ni pamoja na kuitaka serikali iangalie uwezekano wa kuutaifisha mtambo wa kufua umeme wa Kampuni ya IPTL, ambalo Rais Kikwete alisema kwamba jambo hilo ni gumu kwa kuwa litawatia hofu wawekezaji kuja kuwekeza nchini.
Azimio la pili, ni kuiweka wazi mikataba ya umeme, ambalo Rais Kikwete alikubali kuwa itakuwa ikipitiwa na kwamba, serikali itakaa na Bunge kuona namna nzuri ya kutekeleza jambo hilo
La tatu, Takukuru na Polisi kuwachunguza watu waote waliohusika na kashfa hiyo, la nne, kuwawajibisha wenyeviti wa kamati za Bunge walionufaika na mgawo wa fedha hizo.
Azimio la tano, Rais kuunda Tume Kijaji kiwachunguza majaji walionufaika na mgawo wa fedha hizo, akiwamo Jaji Mujulizi na Ruhangisa, ambalo Rais Kikwete alisema katiba na sheria haimpi mamlaka hayo, baliJaji Mkuu, hivyo akataka aachiwe kiongozi huyo wa mahakama.
Azimio la sita, mamlaka za kifedha na kiuchunguzi ziitangaze benki ya Stanbic kuwa ni taasisi yenye shaka katika utakatishaji wa fedha haramu, Rais Kikwete alisema licha ya kuwa azimio hilo ni kali, chombo cha uchunguzi cha Finance Intelligence Unity kimeamza kazi hiyo, hivyo akataka kipewe muda kukamilisha kazi yake.
La saba kuazisha taasisi mahsusi itakayokuwa ikichunguza ufisadi, Rais Kikwete alisema ni wazo zuri, lakini akasema ni vema Takukuru ikapewa uwezo, yakiwamo mafunzo kwa maofisa wanaoajiriwa ili kuwajengea uweledi na uwezo wa kuendesha mashtaka.
Pia kushughulikia masuala ya uongozi na uendeshaji wa taasisi hiyo.
Alhamisi iliyopita Prof. Tibaijuka aliitisha mkutano wa waandishi wa habari ghafla na kusema hawezi kujiuzulu.
Prof. Tibaijuka, ambaye alipata mgawo wa Sh. bilioni 1.6 katika fedha hizo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing LTD, James Rugemalira, alisema kamwe hawezi kujiuzulu na pia anajivunia na kuona fahari kupata fedha hizo. Kampuni hiyo ya Rugemalira ilikuwa mwana hisa katika IPTL.
Alisema ni bora alivyopata fedha hizo na kuzipeleka katika shule yake kwa ajili ya kusaidia shughuli za elimu kwa watoto wa kike wasio na uwezo.
Kutokana na hali hiyo, alisema anahitaji kusifiwa kwa ujasiri wake wa kukiri kupokea fedha hizo na kuzitolea maelezo, ingawa alikosa nafasi hiyo katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Alisema atajiuzulu tu iwapo itathibitika fedha hizo za Rugemalira, siyo halali.
Prof. Tibaijuka alisema fedha hizo hazijathibitishwa na serikali kuwa siyo halali, kiasi cha yeye kutakiwa kujiuzulu nafasi yake serikalini.
Alisema fedha hizo hazina uhusiano kati yake na nafasi ya uwaziri aliyonayo, kwani zilikwenda moja kwa moja kusaidia kulipa deni la Sh. bilioni mbili, ambazo moja ya shule zake ilikopo kutoka Benki M.
Prof. Tibaijuka alisema iwapo itabainika fedha hizo si halali atakuwa tayari kuzirudisha.
“Iwapo fedha hizo zitathibitika siyo halali, Joha Trust itazirudisha, kama taasisi inavyoitwa nia njema, sisi hatuhifadhi fedha zisizo halali,” alisema Prof. Tibaijuka.
Alisema fedha hizo alizipokea Februari 12, mwaka huu, zilitokana na maombi ya awali kutafuta michango kutoka kwa wafanyabiashara wa ndani na wafadhili wa nje.
Alisema hoja kwamba, alipokea mchango mkubwa, haina uzito kutokana aina ya mtu, ambaye alimpaa mchango huo na kusema ni mtu mwenye fedha na pia ni mfanyabiashara.
“Labda mnafikiri unapoomba fedha kwa mtu kama Bill Gates unategemea atakuchangia kama kiasi gani? Siyo senti. Hata mimi nilipoambiwa na Rugemalira nikaangalie akaunti yangu ina shilingi ngapi nakukuta fedha nyingi, nilijua leo nimeamkia mkono wa kulia. Nilifurahi,” alisema Prof. Tibaijuka.
Alisema fedha hizo alichangiwa kwa ajili ya kulipa sehemu ya deni la Sh. bilioni mbili anazodaiwa na Benki M.
Prof. Tibaijuka alisema fedha hizo walikopa kwa ajili ya ujenzi wa bweni la shule lenye uwezo wa vitanda 163.
Alisema fedha hizo zimechangia maendeleo ya elimu kwa kuwatengenezea watoto mazingira bora.
“Hii kitu inabidi tuwe makini kama Taifa, kwani mimi nilikuwa mtumishi Umoja wa Mataifa. Lakini sikuweza kubeba fedha. Na kuna mapesa kule. Iwe katika nchi hii, ambayo nafahamu hata wapigakura wangu wa kule Muleba Kusini na wakulima wanaishi maisha ya chini?” alihoji Prof. Tibaijuka.
Alisema uamuzi wa kuzitoa fedha hizo haraka katika Benki ya Mkombozi, ulifikiwa na Bodi ya Wadhamini ya Joha Trust, ambayo ilitoa maamuzi kwamba, zitumike kulipa deni la Benki M.
Hata hivyo, katika mkutano huo Prof. Tibaijuka hakutoa nyaraka zozote zikiwamo stakabadhi zinazoonyesha deni hilo lilivyolipwa kupitia benki hiyo.
Prof. Tibaijuka alisema analazimika kutoa maelezo hayo katika vyombo vya habari kutokana na kutopewa nafasi ya kufanya hivyo mbele ya PAC.
“Kitendo cha mimi kuitwa Escrow, kwa kweli si kizuri na kinashusha maadili hata ya wewe unayekifanya. Waandishi msiandike, ambacho kinasemwa. Fuatilieni kwa umakini. Kwanza hii inaweza kuliweka Taifa katika image (taswira) mbaya. Nilitumikia Umoja wa Mataifa (UN), hata Katibu Mkuu wa UN akiona nimechukua fedha hizi hii, haipendezi,” alisema Prof. Tibaijuka.
Alisema serikali bado haijathibitisha kuwa fedha za Rugemalira ni haramu kiasi cha yeye kulaumiwa.
Kutokana na hali hiyo, alionya kuwa kujiuzulu kusiwe kama mtindo, kwani fedha hizo hazikugusa utendaji kazi wake kama mtumishi wa serikali.
Alisema mitandao inaendelea kuandika na asilimia kubwa wakimtukana.
CHANZO:
NIPASHE