Mawaziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Profesa Mark Mwandosya (kulia) na Stephen
Wasira (kushoto) wakiteta na Kiongozi wa Upinzani Bugeni, Freeman Mbowe,
Bungeni mjini Dodoma jana Novemba 29, 2014.
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu, William
Lukuvi (kushoto) wakiteta na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe, Bungeni mjini Dodoma jana Novemba 29, 2014.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Profesa Mark Mwandosya (kulia) akizungumza na
Kiongozi wa Upinzani Bungeni Mjini Dodoma jana Novemba 29, 2014.
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na baadhi ya wabunge, Bungeni mjini
Dodoma Novemba 29, 2014. Kulia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Jenista Mhagama.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
I: UTANGULIZI
a) Masuala ya jumla
Mheshimiwa Spika,
1. Leo tunahitimisha shughuli za Mkutano wa Kumi na Sita
na Kumi na Saba wa Bunge lako Tukufu. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi
Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.
Mheshimiwa Spika,
2. Mkutano huu ulijumuisha kujadili kazi kubwa zifuatazo:
Kwanza: Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2015/2016;
Pili: Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa Mwaka 2014 [The Tax Administration Bill, 2014];
Tatu: Muswada wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani wa Mwaka 2014 [The Value Added Tax Bill, 2014];
Nne: Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2014 [The Public Private Partnership (Amendment) Bill, 2014]; na
Tano: Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2014, [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2014].
Aidha, ni hivi mapema leo Miswada 11 ya Sheria ya Serikali kuhusu mambo mbalimbali ilisomwa kwa mara ya kwanza.
Mheshimiwa Spika,
3. Nitumie nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge
wote kwa kushiriki katika Kamati ya Mipango hapa Bungeni kwa kujadili
kwa kina mapendekezo yaliyowasilishwa na Serikali kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2015/2016. Maoni
na Ushauri tuliopokea kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge tutauzingatia
wakati wa maandalizi ya Bajeti ya mwaka 2015/2016. Vilevile, niwashukuru
kwa kujadili na kupitisha Miswada ya Sheria niliyoitaja hivi punde.
b) Maswali
Mheshimiwa Spika,
4. Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge wamepata
fursa ya kuuliza maswali ya kawaida na yale ya Papo Papo kwa Mheshimiwa
Waziri Mkuu. Jumla ya maswali 241 ya msingi na 662 ya nyongeza yameulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Aidha, Maswali 18 ya msingi na 13 ya nyongeza yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
c) Kauli za Mawaziri
Mheshimiwa Spika,
5. Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa tarehe 17
Novemba, 2014 nilipata fursa ya kutoa Kauli ya Serikali kuhusu Mgogoro
kati ya Wakulima na Wafugaji Wilayani Kiteto. Aidha, baadhi ya
Waheshimiwa Mawaziri walipata nafasi ya kutoa Kauli mbalimbali za
Serikali kama ifuatavyo:
i) Kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa kuhusu taarifa zilizotolewa na Vyombo vya Habari za shutuma
dhidi ya Serikali za China na Tanzania kujihusisha na Biashara Haramu ya
Pembe za Ndovu na ile inayohusu Kuridhia Mkataba wa Umoja wa Afrika
kuhusu Demokrasia, Uchaguzi na Utawala wa Mwaka 2007;
ii) Kauli ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii kuhusu Hali ya Dawa Nchini na Matibabu ya Saratani Nchini; na
iii) Kauli ya Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika kuhusu
Mwenendo wa Soko la Nafaka na Mpango wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo.
Maazimio
Mheshimiwa Spika,
6. Tarehe 7 Novemba, 2014 Waheshimiwa Wabunge walipata
fursa ya kujadili na kupitisha Azimio la Bunge la Kumpongeza
Mheshimiwa Anne Semamba Makinda (Mb.), Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa
kuwa Rais wa Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya
ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-PF). Aidha, katika Mkutano
huu Waheshimiwa Wabunge walipata pia fursa ya kujadili na kuridhia
Maazimio mengine yafuatayo:
i) Azimio la Bunge kuhusu Itifaki ya Kuanzishwa kwa Tume ya Utafiti wa Afya, Jumuiya ya Afrika Mashariki;
ii) Azimio la Bunge la Kufuta na Kusamehe Madai au
Hasara itokanayo na Upotevu wa Fedha na Vifaa vya Serikali kwa Kipindi
Kilichoishia tarehe 30 Juni, 2011;
iii) Azimio la Bunge la kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Ushirikiano katika Masuala ya Kiulinzi [The East African Protocol on Cooperation in Defence Affairs]; na
iv) Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Uzuiaji wa
Vitendo Haramu dhidi ya Usalama wa Miundombinu ya Kudumu iliyojengwa
chini ya Bahari katika Mwambao wa Bara ya Mwaka 1988 [The Protocol
for the Suppression of Unlawful Acts Against the Safety of Fixed
Platforms located on the Continental Shelf – SUA, 1988].
e) Taarifa Maalum za Kamati
Mheshimiwa Spika,
7. Mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, Waheshimiwa Wabunge walipokea Taarifa Maalum ya Kamati ya Hesabu za Serikali (Public Accounts Committee - PAC) Kuhusiana na Miamala iliyofanyika katika Akaunti ya “ESCROW” ya TEGETA pamoja na umiliki wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Mheshimiwa Spika,
8. Naomba nitumie fursa hii, kwanza kukushukuru wewe
Mheshimiwa Spika kwa kuruhusu Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC)
kuwasilisha Taarifa hii Maalum kwenye Bunge lako Tukufu kwa mujibu wa
Kanuni za Bunge. Aidha, niwashukuru Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Kamati
kwa uchambuzi wao wa kina na Mapendekezo yao kama yalivyowasilishwa
katika Mkutano huu. Nitumie fursa hii pia kuwashukuru Waheshimiwa
Mawaziri waliozungumza kwa niaba ya Serikali nzima kutoa maelezo
yaliyolenga kutoa ufafanuzi wa hali halisi ya suala hili la Akaunti ya ESCROW ya TEGETA na pia kujibu baadhi ya Hoja za Kamati.
HAPA AMEONGELEA MASUALA YA ESCROW ACCOUNT.
UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA
a) Maandalizi ya Kupiga Kura tarehe 14 Desemba, 2014
Mheshimiwa Spika,
9. Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa Tanzania
Bara unatarajiwa kufanyika tarehe 14 Desemba, 2014. Uchaguzi huo ni wa
kawaida na unahusisha Uchaguzi wa Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji, Mitaa, Wajumbe wa Halmashauri za Vijiji na Wajumbe wa Kamati za Mitaa. Taarifa nilizonazo ni kwamba hadi sasa maandalizi ya Msingi kuwezesha Uchaguzi huo kufanyika yamekamilika.
Mheshimiwa Spika,
10. Ili kuhakikisha kuwa Uchaguzi huo unafanikiwa,
maandalizi ya Kanuni za Uchaguzi yalifanyika kupitia Vikao vya Wadau
mbalimbali ili kupata maoni, mapendekezo na ushauri ambao umesaidia
katika kuboresha Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Wadau
walioshirikishwa ni pamoja na Viongozi wa Vyama vya Siasa vyenye Usajili
wa Kudumu; Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za
Serikali za Mitaa na Asasi Zisizo za Kiserikali (AZAKI).
b) Uandaaji wa Kanuni za Uchaguzi za Mwaka 2014
Mheshimiwa Spika,
11. Katika maandalizi ya awali, orodha ya Vijiji, Mitaa na
Vitongoji iliandaliwa na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali la tarehe
22 Agosti, 2014 lenye Tangazo la Serikali Namba 300 kwa Halmashauri za Miji na Tangazo Namba 301 kwa Halmashauri za Wilaya. Orodha hiyo imejumuisha Kata, Vijiji na Mitaa. Katika Uchaguzi wa mwaka huu, jumla ya Vijiji 12,443, Vitongoji 64,616 na Mitaa 3,741 vitahusika kwenye Uchaguzi.
Mheshimiwa Spika,
12. Ili kufanikisha Uchaguzi huo, Serikali imekwishaandaa
na kuchapisha Vipeperushi, Fomu za Wagombea, Rejesta ya Wapiga Kura,
karatasi za kuonyesha Vituo vya Kupigia Kura, Mabango na Matangazo
mengine kuhusu Elimu kwa Mpiga Kura. Tayari vifaa hivyo vimepelekwa
Mikoani na vingine vinaendelea kupelekwa. Aidha, Masanduku ya Kupigia
Kura yameshanunuliwa na tayari yameshasambazwa katika Mikoa yote
Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika,
13. Kwa vile siku zilizobakia kufikia tarehe ya Kupiga Kura
ni chache, natoa Wito kwa Wananchi ambao hawajajiandikisha katika
Rejesta ya Wapiga Kura wafanye hivyo bila kukosa. Aidha, Viongozi wa
Vyama vya Siasa wawahimize Wanachama wao na Wananchi kwa ujumla
wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na hatimaye wajitokeze siku ya Kupiga
Kura. Aidha, Wasimamizi wa Uchaguzi wahakikishe vifaa vya Uchaguzi
vinafika kwenye maeneo yao kwa wakati.
Mheshimiwa Spika,
14. Napenda nitumie nafasi hii kutoa Rai kwa Viongozi wa
Vyama vya Siasa waendeshe kampeni kwa amani na kuepuka maneno ya
uchochezi, kubaguana kwa misingi ya ukabila, rangi, udini ama hali ya
mtu mambo ambayo yanaweza kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani.
Aidha, nawaomba Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wanachama wao,
wakishapiga kura wasiendelee kukaa katika Vituo vya Kupigia Kura, bali
watawanyike na kusubiri muda wa matokeo.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
15. Leo nimeona nizungumzie masuala muhimu yanayochangia
kusukuma Gurudumu letu la Maendeleo. Kabla sijahitimisha hotuba yangu,
naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha
Mkutano huu. Kipekee nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, pamoja na Naibu
Spika kwa kutuongoza vizuri. Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi
nzuri ya kuongoza vikao vya Bunge lako Tukufu. Aidha, niwashukuru tena
Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri na kwa michango mbalimbali wakati wa
Mkutano huu.
Mheshimiwa Spika,
16. Naomba pia nimshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake
wote pamoja na Wataalam wote wa Serikali na Taasisi zake ikijumuisha
Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na huduma mbalimbali
za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru pia Waandishi wa Habari kwa kazi
nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano na maamuzi
mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru Madereva
kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa
Wabunge, Viongozi mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki
katika Mkutano huu.
Mheshimiwa Spika,
17. Nimalizie kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika majimbo yenu. Aidha,
niwatakie mapumziko mema ya Sikukuu ya Christmas na Mwaka Mpya wa 2015.
Ninaamini kwamba, Mwenyezi Mungu atatulinda na kutuvusha salama sote
kama tulivyo hadi kuuona Mwaka Mpya wa 2015. Baada ya kusema hayo,
naomba sasa kutoa Hoja kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi
tarehe 27 Januari, 2015 saa 3:00 Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa 18 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.
Mheshimiwa Spika,
18. Naomba kutoa Hoja