
Bunge
limefuta pendekezo la Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
lililotaka Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele kuwajibika
kuhusiana na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Bunge
lilifikia uamuzi huo mjini Dodoma baada ya mvutano mkali kati ya
wabunge na Serikali kuhusu utekelezaji wa mapendekezo ya PAC.
Katika
kupitia mapendekezo ya PAC, Serikali ilileta hoja ya kubadilisha
mapendekezo ya kamati hiyo ambayo yalijadiliwa ndani ya Bunge. Bunge
liliazimia vyombo vinavyohusika na uchunguzi kuhusu sakata la Akaunti ya
Tegeta Escrow kuendelea na uchunguzi na vile ambavyo havijaanza vifanye
hivyo ili kubaini ukweli na kuchukua hatua kwa watu wote waliohusika.
Pia,
Bunge liliazimia kuzitaka mamlaka zinazohusika ikiwamo Benki Kuu
kuchukua hatua dhidi ya benki zote zilizohusika na miamala ya Akaunti ya
Tegeta Escrow.
Azimio
jingine ni kuitaka Serikali ifanye mapitio yote ya mikataba ya umeme na
kutoa taarifa bungeni kabla ya kikao kinachofuata cha Bunge kuhusu
utekelezaji wake mapema kabla ya Bunge la Bajeti la mwaka 2015/2016.
Kuhusu
kuiwajibisha bodi ya Shirika la Umeme nchini, (Tanesco), Bunge
liliishauri Serikali ifanye uchunguzi na kuwachukulia hatua wote
waliohusika na kashfa hiyo.
Kuhusu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi kuwajibika
kutokana na sakata hilo, Bunge limeazimia kulifikisha suala hilo kwa
mamlaka ya uteuzi kwa hatua zaidi.
Related Items