
Harbinder Singh Sethi
Sethi ambaye ni muumini mwenzao, ndiye Mwenyekiti wa Makampuni ya Independent Power (IPTL) na Pan African Power Solutions (PAP).
Waumini hao Katika tangazo kwenye vyombo vya habari lililosainiwa na Mwenyekiti wa Shri Guru Singh Sabha Hekalu ya Sikh, Sarbjit Singh, limeeleza kuwa ndani ya sakata hilo kuna uonevu mwingi dhidi ya maazimio yaliyofikiwa na Bunge.
WAMSAFICHA SETHI
Alisema wameamua kuzungumzia suala hilo kwa sababu pamoja na kuingilia imani yao, mmoja wa waumini wa dhehebu lao Sethi wamegundua ameonewa.
“Mimi kama kiongozi wa kiroho, baada ya kuona mmoja wa waumini wangu akitajwa katika sakata hili, nilianza kufuatilia kwa karibu na kumuita Sethi ili nipate ufafanuzi juu ya jambo hili,baada ya maelezo yake na utafiti nilioufanya niligundua kuwa kuna uonevu mkubwa,” alisema na kuongeza:
“Sethi alichukua kiwanda cha kufua umeme cha IPTL mwaka 2013 wakati kikiwa katika hali mbaya ya uzalishaji, kabla ya PAP kuanza uendeshaji wa mtambo huo, uzalishaji umeme ulikuwa ni chini ya megawati 10 na bei ilikuwa inakwenda hadi senti 50 za kimarekani,” alisema.
Alisema mara baada ya Sethi kukabidhiwa mtambo kwa amri ya mahakama iliyotolewa na jaji Mtamwa wa Mahakama Kuu ya Tanzania, mfanyabiashara huyo aliweza kuzalisha megawati hadi 100 na bei ilifikia senti 23 za kimarekani.
“Kwa historia hii fupi, tunaona uwezekano wa wafanyabiashara wenzake kuwa na wivu na kinyongo kwa sababu ameweza kuzalisha umeme mwingi na kwa bei nafuu kwa Watanzania, pia mazingira ya sakata hili yana kila dalili za mwingiliano wa kisiasa na uchu wa madaraka, kuna watu wanataka kuchafua sifa za viongozi kwa nia ya kujinufaisha,”.
SINGA SINGA
Alisema waumini wa dhehebu hilo waishio na kuabudu katika hekalu za Tanzania, wamekuwa wakisikia na kusoma katika vyombo vya habari, kutumikia jina la Singa Singa kutambulisha waumini wa dhehebu lao.
Alisema kitendo cha kumuita muumini wa dhehebu la Singh kwa jina la singa singa ni kuingilia uhuru wao wa kuabudu kwani ni neno la kuashiria dharau na tusi kwao. Katika tangazo hilo, waumini hao wamesema kuwa watachukua hatua kwa yeyote atakayeendelea kutumia lugha ya kejeli kwao.
Aidha, wameeleza kuwa wameishi nchini kabla ya uhuru huku wakijihusisha na biashara mbalimbali ikiwemo kilimo, ujenzi, ufuaji chuma, masuala ya umeme na wamekuwa wakifanya kazi za kitaalam.
Katika tangazo hilo mwenyekiti huyo, alisema ni vyema mtu akaitwa kwa jina lake ili kuondoa dhana ya ubaguzi ambayo waasisi wataifa waliweka misingi mizuri ya kuiondoa. Alisema neno singa kwenye kamusi mbalimbali lina maana ya kitu cha ajabu, kitu chenye nguvu ya ajabu za kimiujiza.
MASABURI
Wakati huo huo, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, amejitosa katika sakata la akaunti ya Escrow na kueleza kuwa kumekuwa na upotoshaji mkubwa ambao unahatarisha kuligawa taifa.
Alisema anayepaswa kulaumiwa katika hilo ni Kampuni ya Mechmar kwani ndiye chanzo cha matatizo yote ambayo yametokea.
Dk. Masaburi amesema mjadala kuhusu sakata hilo umepotoshwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya watu hususani wanaojua ukweli, hivyo kusababisha taharuki na kutoaminika.
Dk Masaburi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (Alat), aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa tawala za mitaa.
Alisema hivi sasa taifa linashuhudia kasi ya upotoshwaji unaofanywa na watu wachache na wapo ambao wanalifahamu sakata hilo lakini matokeo yake wanawapotosha umma.
Dk Masaburi, alisema kiasi cha fedha kinachoelezwa kwa umma kwamba ‘kimechotwa’ kupitia akaunti ya Escrow kinapotoshwa kwa makusudi pasipo kuelezwa ukweli wa kuwapo malipo halali yaliyotokana na matumizi ya umeme.
“Unapoeleza kwa umma kwamba fedha zote zilizokuwa kwenye akaunti ya Escrow zingeweza kutumika kwa miradi fulani ya maendeleo ni upotoshaji kwa maana miongoni mwa hizo zimo zilizostahili kulipwa kutokana na nishati ya umeme iliyotumika,” alisema.
Alisema badala yake wametokea watu wa aina tatu wakiwamo wanataaluma wanaolifanya suala la akaunti ya Escrow kutoeleweka kutokana na kuupotosha umma.
Kwa mujibu wa Dk Masaburi, wanataaluma wamejenga imani kwa baadhi ya watu wanaoamini kwamba kiasi cha zaidi ya Sh. Bilioni 300 zilizokuwa kwenye akaunti hiyo, zilichukuliwa kwa njia haramu.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI