POLISI MBARONI KWA KUWASINDIKIZA NCHINI WAHALIFU WA KENYA.

By | 13:23

Polisi mkoani Kilimanjaro imewatia mbaroni askari polisi sita wa Kituo cha Polisi Himo kwa tuhuma za kuwasindikiza wahalifu kutoka nchini Kenya na kuingia Tanzania kinyume cha sheria.

Imedaiwa kuwa wahalifu hao ni wezi wa magari walioingia nchini na kukamatwa na baadaye kuwahonga polisi hao na kuachiwa kabla ya kukamatwa tena mjini Moshi.

Wahalifu hao imedaiwa walikuwa na magari mapya mawili kutoka nchini Kenya  yaliyokuwa hayana kibali cha Mamlaka ya Mapato (TRA), Bima, wala vibali vya kuingia nchini.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwella na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama, wamethibitisha kuwepo kwa tukio hilo jana walipoongea na NIPASHE kwa njia ya simu.

Kamanda Kamwella, alisema hawezi kuwataja majina kwa sasa kwa kuwa upelelezi bado  unaendelea.

"Ni kweli tunawashikilia ila ni mapema kuelezea tukio hilo,” alisema.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alisema polisi watatoa taarifa kuhusu tukio hilo.
Taarifa kutoka kamati ya ulinzi na usalama mkoani hapa, zimeeleza kuwa matukio ya polisi kuwasindikiza wahalifu au kuwakamata na kuwaachia ni matukio ya kawaida.

Imedaiwa kuwa baadhi ya askari hao wa kulinda mpaka wa nchi wamekuwa wakikamata mirungi, madawa ya kulevya, mafuta ya taa, kusindikiza wasomali na kupewa fedha kuanzia Sh. 10,000 hadi Shilingi milioni tano kulingana na ukubwa wa kosa.

Baadhi ya wadau, walidai kuwa endapo serikali haitalisimamia jeshi la polisi kwa kuwapatia masilahi yao muhimu, itafikia mahali wahalifu wa kigaidi watapishwa kwa njia za panya.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu, akiongea na NIPASHE kwa njia ya simu alisema kuwa licha ya mapungufu yaliyopo ya kifedha jeshi hilo litaendelea kuwalinda wananchi na mali zao na kutetea weledi wa jeshi hilo na maadili ya kipolisi.
 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Newer Post Older Post Home