Pia yumo Bosi TRA, kufika mbele ya Kamati ya PAC, Zitto asema fedha hizo zipo za watu binafsi, kampuni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe.
Kwa mujibu wa Zitto, PAC imewaita Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof.
Benno Ndulu; Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk. Rished Bade, ili
kuhojiwa na kamati yake Machi 9, mwaka huu. Akizungumza na NIPASHE jana
jijini Dar es Salaam, Zitto alisema majina ya watu au kampuni
zinazohusika na mabilioni hayo vitajulikana kwa kuwa serikali
imeshachunguza na ripoti iko tayari.
“Tumewaita BoT, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna Mkuu wa
TRA Machi 9 waje kwenye kamati kujieleza…tunategemea serikali ina
taarifa zote kwa sababu sehemu kubwa ya fedha zinazotoroshwa nje ni kwa
nia ya kukwepa kodi. Kwa hiyo, TRA watakuwa wanawajua,” alisema Zitto.
Aliongeza: “Siwezi kumtaja mtu yeyote kwa sasa. Lakini bila shaka wahusika wakuu watakuwa wafanyabiashara wakubwa.”
Kwa upande wake, Prof. Ndulu aliliambia NIPASHE kuwa ameitwa na
PAC, lakini hawezi kuueleza umma taarifa zozote kwa sasa kwa kuwa
atajieleza kwenye kamati.
“Subirini, mimi nimeshaitwa kwenye kamati. Nitajieleza huko…unataka
niseme nini sasa hivi wakati nitahojiwa huko?” Alihoji Prof. Ndulu.
Tuhuma za vigogo wa Tanzania kuficha mabilioni ya shilingi katika
benki za Uswisi ziliibuliwa upya hivi karibuni baada ya ripoti ya
mtandao wa Swiss Leaks chini ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi wa
Kimataifa (ICIJ), kutaja vigogo 99 wenye akaunti za siri nchini humo.
Taarifa ya Swiss Leaks iliyotolewa mapema mwezi huu ilieleza kuwa
vigogo hao wa Tanzania wana akaunti za siri zenye Dola za Marekani
milioni 114, ambazo ni sawa na Sh. bilioni 194.
Msingi wa ripoti hiyo ulitokana na aliyekuwa mfanyakazi wa Benki ya
Kimataifa HSBC, Hervé Falciani, kuvujisha siri za akaunti za wateja
baada ya kuacha kazi; na mwaka 2008, alivujisha siri za akaunti za siri
za baadhi ya watumishi wa umma na wanasiasa kwa Serikali ya Ufaransa
ambayo mamlaka za kodi nchini humo ilifanya uchunguzi na kuthibitisha.
HSBC ni benki kubwa ya biashara duniani ambayo ilianzishwa mwaka 1836.
Kwa mujibu wa Swiss Leaks, matokeo ya uchunguzi huo yanatokana na
aina tatu za taarifa ndani ya benki kwa vipindi tofauti; Mosi ni
taarifa za wateja na uhusiano wao na akaunti za benki nchini Uswiss kwa
kipindi cha kuanzia mwaka 1988 hadi 2007.
Pili, ni picha kamili ya kiasi cha juu cha fedha kilichokuwapo
kwenye akaunti ya mteja katika kipindi cha mwaka 2006 na 2007 na tatu,
ni mawasiliano kati ya mteja husika na wafanyakazi wa benki katika
kipindi cha mwaka 2005.
Ripoti hiyo ya Swiss Leaks, inaeleza kuwa taarifa za kiuchunguzi
kutoka kwenye benki nchini Uswiss zinaonyesha kuwa akaunti hizo
zinahusishwa na baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa na
watumishi wa umma ambao wamejipatia utajiri wa siri unaotokana na
kampuni hewa (offshore companies).
Hata hivyo, ICIJ haikutaja majina ya Watanzania wenye akaunti hizo
badala yake walieleza kuwa baadhi ya wateja wanaweza kuwa na akaunti
nyingine zaidi nje ya Uswiss au kwenye nchi mbalimbali. Ripoti hiyo pia
inaeleza kuwa akaunti za siri kwenye mabenki unafanyika kwa makusudi
ukiendeshwa na mtandao ukihusisha mamlaka mbalimbali.
Ripoti hiyo pia iliitaja Kenya kama kinara kwa nchi za Afrika
Mashariki ikiwa na wateja 742 wenye akaunti za siri zenye Dola za
Marekani milioni 559.8.
Tanzania ni ya pili, ikifuatiwa na Uganda yenye wateja 57 wenye
akaunti zenye Dola za Marekani milioni 89.3 na Burundi ni ya mwisho kwa
kuwa na wateja 11 wenye Dola za Marekani milioni 29.4.
Tuhuma za kuwapo kwa vigogo wenye akaunti za siri nchini Uswiss ziliibuliwa na Zitto bungeni mwishoni mwa mwaka 2012.
Baada ya kuibuka kwa sakata hilo mwaka 2012 na Bunge kuiagiza
serikali kufuatilia, serikali haijaomba taarifa yoyote kutoka Uswisi
kuhusu Watanzania waliohifadhi fedha nchini humo.
Mwaka jana, Zitto alikaririwa akisema kuwa wapo watu waliopata
fedha kihalali, lakini wanaficha fedha hizo na mali zao nje ili kukwepa
kodi na wengi wa hao ni wafanyabiashara wakubwa nchini.
Alisema pia kuwa Tanzania imepoteza Dola za Marekani 1.25 bilioni kati ya mwaka 2001 na 2012 kwa njia hizo.
Kufuatia hoja hiyo ya Zitto, Serikali iliunda timu kutokana na
Azimio la Bunge lililotolewa mwishoni mwa mwaka juzi ambayo ilikuwa
inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Viongozi wengine wanaounda tume hiyo ni Mkurugenzi wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea, Mkurugenzi
wa Usalama wa Taifa, Othman Rashid na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa
Benno Ndulu.
CHANZO:
NIPASHE