
Kampuni ya Tullow Oil imesema kuwa itailipa serikali ya Uganda dola milioni 250 baada ya kuafikiana kuhusu mgogoro wa kodi kwa muda mrefu.
Pande hizo mbili zilienda mahakamani nchini Uganda na Uingereza kuhusu swala hilo.
Kodi imekuwa swala kuu kati ya serikali na kampuni za mafuta zinazofanya kazi nchini humo.
Kampuni ya Tullow Oil imekuwa ikipinga kiwango cha kodi inachopaswa kulipa kufuatia makubaliano ya dola bilioni mbili iliotia sahihi na kampuni ya Total na China CNOOC kuingia katika makubaliano nchini Uganda.
Kampuni hiyo ilipoteza kesi mbili mjini Kampala na katika mahakama ya kimataifa ya kutatua mizozo lakini ikakata rufaa.

Mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini Uganda URA iliitaka kampuni hiyo kulipa dola milioni 437 lakini kampuni hiyo ikakataa.
Sasa kampuni hiyo italipa dola milioni 250 ili kumaliza kusitisha makabiliano yote ya mahakamani.
Serikali na kampuni za mafuta zinajadiliana kuhusu kandarasi ambazo zitaifanya Uganda kuanza kuzalisha mafuta.
Kiwango cha kodi inayotozwa kimekuwa swala nyeti katika mazungumzo hayo.