JK:TUNABORESHA JESHI ILI KULINDA MIPAKA.

By | 11:02


RAIS Jakaya Kikwete amesema Tanzania inaimarisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), siyo kwa nia ya kumchokoza mtu ama nchi yoyote, bali kwa nia ya kulinda mipaka yake kwa sababu kila hatua ya maendeleo ina changamoto tofauti za ulinzi wa nchi.
Aidha, amesema kuwa siyo uharibifu kutumia fedha nyingi kujenga jeshi kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wanadai, kwa sababu ni wajibu wa kila nchi kuhakikisha kuwa jeshi lake linakuwa katika utayari wa kukabiliana na uchokozi wa aina yoyote.
Rais vile vile amesema uchumi wa Tanzania, na hasa uchumi mpya wa gesiasilia, ambayo ndiyo itakuwa msingi mkuu wa uchumi na maendeleo ya Tanzania lazima ulindwe kwa njia yoyote na kwa nguvu zote.
Rais Kikwete aliyasema hayo juzi wakati alipozungumza katika Sherehe ya Kukamilisha Mradi wa Ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kurushia Ndegevita na Sherehe ya Kufungua Mradi wa Kuongeza Urefu wa Uwanja wa Ndegevita katika Kituo cha Kijeshi cha Kamandi ya Anga cha Ngerengere, Mkoa wa Morogoro.
Rais aliwaambia walioshuhudia sherehe hiyo akiwemo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Ali Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini, Dk Lu Youquing kuwa Tanzania inajenga jeshi lake vizuri kwa ajili ya ulinzi wa mipaka yake. “Na wala tusije kujidanganya.
Kutumia fedha nyingi kujenga jeshi letu siyo ubadhirifu wa fedha. Ni jambo la lazima kabisa. Ni matarajio yangu kuwa sera za namna hiyo zitaendelea, hata chini ya uongozi ujao, hata kama baadhi ya watu wanaweza hata wakaanza kufikiria sera ya kupunguza matumizi ya kijeshi… Yatakuwa ni makosa makubwa,” aliongeza Amiri Jeshi Mkuu.
Rais Kikwete pia aliishukuru nchi ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuisaidia Tanzania katika masuala ya ulinzi, akisisitiza kuwa katika ujenzi wa Jeshi la Tanzania hakuna nchi rafiki kama China duniani. “Ni wajibu wetu kuwajua na kuwashukuru marafiki zetu wa kweli,” alieleza.
China ndio inagharimia miradi hiyo miwili ya maboresho ya Uwanja wa ndegevita wa Ngerengere ambao ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia hata ndege kubwa za abiria ikitokea hali ya dharura katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wa Dar es Salaam.
HABARI LEO.

Newer Post Older Post Home