MCHUNGAJI MTIKILA KUAGWA DAR LEO,ANAYEKAIMU KUENDELEZA KESI ZAKE.

By | 03:56




Mchungaji Mtikila
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, anatarajiwa kuagwa leo katika ukumbi wa Karemjee jijini Dar es Salaam na kusafirishwa kuelekea mkoani Njombe kwa mazishi.

Mchungaji Mtikila alifariki dunia Oktoba 4, mwaka huu kwa ajali ya gari katika kijiji cha Msolwa, Chalinze mkoani Pwani akitokea mkoani Njombe kwenye kampeni za uchaguzi za wagombea wa chama chake wa nafasi za udiwani na ubunge Jimbo la Njombe Kusini.

Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu, Stanley Mtikila, taratibu za kuuaga mwili wa marehemu Mtikila zilishaanza jana usiku nyumbani kwa marehemu, Mikocheni ‘B’ jijini Dar es Salaam.

Alisema mwili wa marehemu ambao ulichukuliwa jana kutoka Hospitali ya Jeshi Lugalo ulikokuwa umehifadhiwa baada ya kuhamishiwa ukitokea katika Hospitali Teule ya Tumbi, Kibaha na kulala nyumbani kwake, utaanza kutolewa heshima za mwisho nyumbani kwake leo saa 2:00 asubuhi.

Alifafanua kuwa taratibu za kuuaga mwili huo zitatanguliwa na salamu za rambirambi kutoka kwa wawakilishi wa makundi mbalimbali na viongozi mbalimbali wa serikali, wawakilishi wa DP na Liberty International Foundation.

“Tunatarajia kuondoka kesho mchana (leo), kuelekea kijiji cha Milo Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe kwa mazishi,” alisema.

MRITHI KUENDELEZA KESI
Kwa upande wake, Msemaji wa chama ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa DP, Abdul Mluya, alisema wataendeleza na kuyaenzi yote aliyoyaacha marehemu kwa manufaa ya chama chao na taifa.

Alisema watahakikisha wanaenzi Utanganyika pamoja na kufichua maovu pamoja na kuwa watetezi wa Watanzania.
“Tunatarajia kuendelea pale alipoishia Mwenyekiti wetu kuhakikisha tunayaenzi aliyoyaacha na kufuata nyayo zake ikiwa ni pamoja na kuuenzi Utanganyika,” alisema Mluya.

Anayekaimu nafasi ya Mtikila ni Makamu Mwenyekiti wa DP Zanzibar, Peter Mapwila, alisema wanatarajia kuendeleza kesi zote alizozianzisha katika mahakama mbalimbali nchini.

Alisema mfano wa kesi mbili ambazo wanazifanyia kazi ni ya Mchungaji Mtikila kuzuiwa kuwania nafasi ya urais pamoja na ile aliyomfungulia mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, kufanya kampeni kabla na wakati akiwa CCM.
SOURCE:TUBONGE TZ.
Newer Post Older Post Home