
Uchaguzi mkuu Tanzania utafanyika Oktoba 25, mwaka huu, wakati wa Uganda utafanyika robo ya kwanza ya 2016.
Kidega alisema hayo wakati wa kuanza kwa mkutano wa pili, kikao cha nne cha Bunge la tatu la Eala kilichoanza jijini Nairobi juzi na nakala ya hotuba yake ilipatikana makao makuu ya EAC mjini Arusha jana.
“Ombi letu kwa nchi wenzetu wanachama ni kuhakikisha chaguzi zao zinafanyika kwa ustaarabu na mchakato huo lazima uzingatie Katiba na sheria za uchaguzi,” alisema.
Aidha, Kidega alitoa changamoto kwa vyombo vya habari kuhakikisha vinazingatiaweledi na maadili ya kazi zao bila kuumiza upande wowote.
“Vyombo vya habari vinatakiwa kuzingatia maadili, vinatakiwa kuacha kuchochea mihemko kwa jamii isipokuwa kuhamasisha uchaguzi huru, wa amani na wenye kuzingatia haki na ustaarabu,” alisema na kuongeza:
“EAC inasimamia umuhimu wa kuwa na chaguzi huru, zenye kuzingatia haki na sheria katika kujenga demokrasia,” alisema.
Kidega aliongeza kusema kuwa suala la amani na usalama wa nchi wanachama linapewa kipaumbele na Jumuiya ya Afrika Mashairiki (EAC) licha ya kuwapo kwa vitisho vya ugaidi.
CHANZO: NIPASHE