TUME YA TAIFA UCHAGUZI KUFIKISHWA TAKUKURU.

By | 05:13


  Vinara manunuzi yenye rushwa ya mabilioni hawa hapa...
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Huhu zikiwa zimebaki siku 17 kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepata pigo la aina yake baada ya kutajwa kuwa ni miongoni mwa taasisi tisa vinara zenye manunuzi yaliyojaa viashiria vya rushwa na hivyo kuwa mbioni kufikishwa kwenye Taasisi ya Kuchunguza na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kabla hatua zaidi hazijachukuliwa.
Taarifa iliyotolewa jana na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kuhusiana na ripoti yake ya mwaka 2014/2015, inaonyesha kuwa NEC inakabiliwa pia na kashfa ya manunuzi mabaya na hivyo kuwamo katika kundi la Taasisi 17 zinazotajwa kuwamo katika eneo hilo. 
Hali hiyo imeibuliwa ikiwa ni kipindi kifupi tu kimepita baada ya Nec kutaja gharama za awali kwa ajili ya vifaa mbalimbali kama wino, fulana, kofia, karatasi za kura, vibanda vya kupigia kura na vifaa vinginevyo kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kufikia Sh. bilioni 31.25. 
Hata hivyo, haikuelezwa zaidi kama ripoti hiyo ya PPRA inahusisha moja kwa moja manunuzi ya vifaa na maandalizi mengine yanayohusiana na uchaguzi huo ambao hivi sasa upo katika hatua ya kampeni ili  kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake baada ya uchaguzi.
Mwenyekiti wa bodi ya PPRA, Balozi Matern Lumbanga, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya ripoti ya ukaguzi wa manunuzi ya umma ya PPRA waliyoifanya kwa kipindi hicho cha mwaka 2014/15.
Alisema tathmini ya jumla ya viashiria vya rushwa inaonyesha kwamba kati ya taasisi 80 za umma zilizokaguliwa, tisa ikiwamo NEC, ndizo zilizopata wastani wa asilimia 20 au zaidi ambavyo ni vya juu vya rushwa kwa mujibu wa vigezo vyao. Wastani wa jumla wa viashiria vya rushwa kwenye taasisi hizo tisa ni asilimia 24.95.
Aliongeza kuwa viashiria hivyo vilionekana kwa kiwango kikubwa kwenye eneo la usimamizi wa mikataba mbalimbali, ambalo lilikuwa na kiwango cha asilimia 36.
Alizitaja taasisi hizo tisa kuwa ni Halmashauri ya Wilaya ya Karatu iliyoongoza kwa kuwa na asilimia 31, NEC inafuatia kwa kuwa na viashiria vya juu vya rushwa vya asilimia 29 na nyingine ni Agricultural Input Trust Fund asilimia 28, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma (28%), Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo (24%), Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda (22%), Kampuni ya Reli (TRL) asilimia 22, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni 21% na Halmahauri ya Wilaya ya Mbozi asilimia 20.
Lumbanga alisema kufuatia ripoti hiyo, hatua ya kwanza watakayochukua ni kupeleka ripoti yao Takukuru ili uchunguzi ufanyike na mwishowe hatua zaidi zichukuliwe pindi ikionekana ipo haja ya kufanya hivyo.
“Tutapeleka ripoti Takukuru ambao wao ndiyo wenye mamlaka ya kuchunguza zaidi. Sisi hatuwezi kutoa taarifa zaidi ya ripoti hii hadi pale uchunguzi utakapokamilika.    
Kwa hiyo, kuhusu taarifa zaidi juu ya kilichofanyika NEC na hata taasisi nyingine, subirini hadi uchunguzi utakapokamilika,” alisema Lumbanga.
Aidha, Lumbanga alisema ripoti hiyo ya PPRA imebaini vilevile kuwa taasisi 17 zimefanya vibaya katika ununuzi pamoja na kuwa zilishakaguliwa miaka ya nyuma na kupewa mapendekezo ya namna ya kuboresha manunuzi yao kwa mujibu wa sheria.
Ripoti inaonyesha kuwa taasisi hizo na alama walizopata kuwa ni Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda (42), NEC (38), Halmashauri ya Wilaya ya Karatu (49), Tume ya Ajira (53), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (51), Stamico (56), Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi (50), Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo (57) na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma (52).
Nyingine ni Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi (55), Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (56), Kampuni ya Reli Tanzania (51), Halmashauri ya Wilaya ya Iramba (52), Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu (60), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (60), Halmashauri ya Wilaya ya Kyela (60) na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Lindi (60).
UCHELEWESHAJI MALIPO TANROADS
Mbali na kubaini taasisi zenye manunuzi yenye viashiria vya rushwa, Lumbanga alisema wamebaini kuwapo kwa ucheleweshwaji mkubwa wa malipo kwa wakandarasi kwenye miradi ya ujenzi wa barabara nchini, chini ya Wakala wa Barabara (TANROADS) na miradi ya maji kwenye serikali za mitaa.
Alisema jumla ya mikataba 301 ya TANROADS yenye thamani ya Sh. trilioni 5.3 ilicheleweshwa malipo na hivyo kusababisha malimbikizo ya riba ya Sh. bilioni 124.8 hadi kufikia Juni, 2015; pamoja na kuwapo kwa malipo hewa ya Sh. milioni 377.
Aliongeza kuwa wamebaini kuwapo kwa taasisi tisa zilizofanya malipo kwa kazi au manunuzi ambayo hayakufanywa kabisa, huku miradi yenye thamani ya Sh. bilioni 6.4 ikibainika kuhusika na malipo ya aina hiyo pia. 
Aliongeza kuwa wamebaini kuwapo kwa malipo ya ziada ya Sh. milioni 951.7 yaliyolipwa kwa wakandarasi kwa kazi hewa.
Alizitaja taasisi hizo na kiasi kilicholipwa kama malipo ya ziada kwenye mabano kuwa ni Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma (Sh.milioni 11.), Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo (Sh. milioni 64.9), Halmashauri ya Jiji la Mwanza (Sh. milioni 69.6) na Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi (Sh. milioni 55.6).
Taasisi nyingine ni Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Sh.milioni 25.42), Tanapa (Sh.milioni 156.3), Kampuni ya Reli Tanzania (Sh.milioni 473.6), Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe (Sh.milioni 93.09) na Halmashauri ya Wilaya ya Kyela (Sh. milioni 1.08).
HATUA ZILIZOCHUKULIWA 
Lumbanga alisisitiza kuwa ripoti zao za ukaguzi za taasisi ambazo zimebainika kuwa na viashiria vya rushwa kwa asilimia zaidi ya 20 zitawasilishwa kwa uchunguzi zaidi na kwamba, wakuu wa vitengo vya manunuzi waliohusika katika makosa hayo watalazimika kujieleza mbele ya bodi ya wakurugenzi wa PPRA.
Alitaja hatua nyingine kuwa ni taasisi zilizopata wastani wa chini ya asilimia 75 kutakiwa kuwasilisha PPRA mahitaji yao ya mafunzo kuhusu sheria ya manunuzi na kanuni zake.
Alisema kuhusiana na malipo kwa wakandarasi kwa kazi ambazo hazikufanywa, PPRA itapeleka timu ya wataalamu kuhakiki malipo hayo na timu hiyo itahusisha wakandarasi na wataalamu washauri waliohusika na miradi hiyo, meneja wa miradi na taasisi husika.
Aliongeza kuwa taasisi zitakazobainika kuwa zilifanya malipo kwa kazi ambazo hazikufanyika (malipo hewa) zitatakiwa kurejesha fedha hizo kutoka kwa wazabuni waliolipwa.
KAMPUNI ZAFUNGIWA
Kadhalika, PPRA imezifungia kushiriki zabuni za umma kampuni saba pamoja na wakurugenzi wake kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kukiuka mikataba waliyoingia na taasisi mbalimbali za umma na vitendo vya udanganyifu na pia kuwasilisha dhamana za zabuni za kughushi wakati wa michakato ya zabuni.
CHANZO: NIPASHE
Newer Post Older Post Home