
Kundi la wapatanishi wa mazungumzo nchini Tunisia limetunukiwa tuzo ya Nobel ya mwaka huu kwa jukumu lao la kufanikisha demokrasia nchini humo.
Akitangaza waliopewa tuzo hiyo ,mwenyekiti wa kamati ya Nobel amesema kuwa kundi hilo la watu wanne lilitoa mchango mkubwa kwa ujenzi wa demokrasia baada ya maandamano ya mwaka 2011.
Wapatanishi hao walikuwa miongoni mwa wagombea 273 walioteuliwa kuwania tuzo hiyo.Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na papa francis ni miongoni mwa wale waliotarajiwa kushinda.
Wapatanishi hao wanne walitoka katika mashirika manne ikiwemo muungano wa wafanyikazi nchini Tunisia,Shirikisho la viwanda,biashara na haki za binaadamu,vyama vya haki za kibinaadamu pamoja na chama cha mawakili.
''Mashirika haya yanashirikisha sekta tofauti za maadili katika jamii ya raia wa Tunisia.Maisha ya ajira,maslahi,sheria na haki za kibinaadamu'',alisema mwenyekiti wa kamati hiyo Kaci Kullmann Five.
Ni kutokana na hilo ndiposa wanne hawa walichukua majukumju yao kama wapatanishi ili kusukuma gurudumo la demokrasia na maendeleo nchini Tunisia kwa ari na maadili ya hali ya juu.