Wasomi: Tunahitaji rais ajae awe dikteta.

By | 14:00

Dar es Salaam. Baadhi ya wananchi wamekuwa na maoni tofauti kuhusu namna sakata la
 wizi wa fedha kwenye akaunti ya Escrow linavyoshughulikiwa, huku wengine wakisema
 umefika wakati sasa nchi iongozwe na rais dikteta.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, walisema kuwa uamuzi wa Naibu Spika,
Job Ndugai kuwaomba wabunge kukishauri kiti chake juu ya hatua ya kuwasilishwa na
kujadiliwa kwa ripoti ya uchunguzi wa fedha za Escrow, umeonyesha Bunge linataka ukweli ujulikane.
Mratibu wa Umoja wa Wanawake  Wanasiasa Tanzania (ULINGO), Dk Ave Maria Semakafu
alisema baadhi ya watu wanataka kupotosha ukweli kwa kuwataja viongozi wasiohusika hawahusiki
 moja kwa moja na ufisadi wa fedha hizo badala ya kuwanyooshea kidole majaji waliotajwa kupewa
 mgawo huo.
Akizungumzia suala la mahakama kuzuia jambo hilo kujadiliwa bungeni, alisema kinachofanyika ni
sawa na kumpa nyani kesi ya ngedere huku ukijua kabisa haki haitotendeka.
“Hata waandishi wa habari wanakosea mahali  pa kulenga, majaji watatu ndio wametajwa kupata
mgawo (anawataja), suala hapa Jaji Kiongozi atoe taarifa kuhusiana na jambo hilo,” alisema Semakafu.
Alisema kutokana na kujirudiarudia kwa matukio ya ufisadi nchini, taifa limepoteza mwelekeo hivyo
linahitaji kiongozi dikteta atakayeweza kuwashughulikia wahalifu bila huruma.
“Nchi haijulikani inakwenda au inarudi. Dawa ni kupata kiongozi dikteta, nchi hii haihitaji mtu mwenye
makundi, tumefika hapa kwa sababu ya urafiki,” alisema Semakafu.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho alisema
 kinachoonekana sasa ni matokeo ya viongozi kutokuwa na utamaduni wa kuchukua hatua
kali watu wanapofanya makosa, ikiwamo kufilisi mali zao.
Profesa huyo alisema kwa hali ilipofikia nchi inahitaji kupata kiongozi dikteta ambaye atakuwa
tayari kutawala kwa muda mfupi ili arudishe nidhamu iliyopotea.
“Tunahitaji dikteta atakayesema nitakaa kwa muda mfupi, asafishe uozo, kisha aondoke…
, Haiwezekani tuendelee kushuhudia nchi ikizidi kufilisika,” alisema Profesa Shumbusho.
Mbunge wa Mgogoni, Kombo Khamis Kombo (CUF), alisema matukio ya ufisadi
yameongezeka nchini kwa sababu kila kiongozi anayetarajiwa kuchukua hatua analalamika
 kuwa watendaji wake wanamwangusha.
“Viongozi wanapiga danadana, wana watu ambao hawawezi kuwakosoa…, tulipofikia tunahitaji
kiongozi mwenye maadili,” alisema Kombo.

Mkuu wa Kitivo Msaidizi  (Taaluma), Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii,  Chuo Kikuu cha
Tumaini Dar es Salaam, Danford Kitwana alisema kilichotokea bungeni juzi kinaashiria Serikali
kujaribu kulizima suala la Escrow ili lisijadiliwe kwa kuwa wanafahamu linaweza kuwang’oa baadhi
 ya viongozi madarakani.
Hata hivyo, alisema kutokana na kauli za wabunge wengi waliotoa mapendekezo yao kutaka jambo
hili lijadiliwe na ukweli kufahamika, Serikali itakuwa na nafasi ndogo ya kukwepa kutekelezwa kwa
 maoni ya wabunge walio wengi.
Aliongeza: “Tatizo la Tanzania ni ukosefu wa maadili na uchungu wa mali ya umma, tutaendelea tu
kusikia kesi kama hizi kwani bado kuna mambo mengi yaliyofanywa bado hayajafichuliwa.”
Newer Post Older Post Home