
Aidha, vijana hao wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwaondoa madarakani wale wote waliohusika na upotevu wa fedha hizo huku wakimtaka kuacha kushughulikia matatizo madogo, bali ashughulikie yale ambayo yamekuwa yakiwaumiza Watanzania.
Akizungumza katika mkesha wa kuukaribiasha mwaka mpya wa 2015 katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Chuo cha Mipango mjini hapa, Makamu Mwenyekiti wa Jumuia ya Vijana wa Kikristo Dodoma, Emmanuel Matonya, alisema Rais anatakiwa atoe mfano kwa waliohusika ili wawengine waogope.
“Wanavyuo wa Dodoma tunataka Rais awafukuze kazi wale wote waliohusika na uchotwaji wa fedha za Escrow,pamoja na kufilisiwa mali zao kwani tunatakiwa tuwe waaminifu kwa wale waliotuamini, na sisi ambao tupo huku vyuoni tuwe na woga pale tunapopewa madaraka,” alisema Matonya.
‘’Sisi kama wasomi tunaona uadilifu na maadili ya viongozi wetu yanatupa maswali magumu, sisi wasomi kuna shida gani, mbona mambo madogo yanashughulikiwa, lakini makubwa yamekuwa ni tatizo?” alihoji na kuongeza
“Tunamuomba Rais ayashughulikie haya hasa mwaka huu wa uchaguzi kwani kila mtu anataka amani.”
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mnadani, ambaye pia alikuwa ni mgeni Rasmi katika mkesha huo, Steven Masangia, aliwataka vijana kuliombea Taifa kwa mwaka 2015 waache kuiba fedha za walipa kodi wa nchi hii kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanarudisha maendeleo ya nchi nyuma.
Masangia alitoa wito kwa vijana hao kuliombea Taifa amani na utulivu na kuachana na viongozi wa kisiasa ambao wanataka kuwagawa huku akitolea mfano kwa Palestina na Israel jinsi zilivyotumia muda mrefu kusaka amani bila mafanikio.
‘’Naomba kuwasihi nyinyi vijana mzidi kuliombea Taifa letu amani kwani huu mi mwaka wa uchaguzi mkuu, Yesu alipokutana na vijana wake alisema nawapeni amani, hivyo ni kitu kikubwa tuchonatakiwa tukienzi,’’ alisema.
CHANZO:
NIPASHE