Polisi wakipambana na magaidi hao.
Kwa mujibu wa baadhi ya wakazi wa Vijiji vya Mafuriko, Mikocheni,
Majimoto, Kilomoni na Amboni yenyewe, wanaamini wahalifu hao ni
makomandoo wazuri na waliishi kwenye mapango hayo wakijua siku
wakivamiwa watapambana vikali.
KWA NINI MAKOMANDOO?
Mkazi
mmoja wa Kijiji cha Majimoto alisema kwa jinsi watu hao walivyofanikiwa
kutoweka katika mazingira tata huku wakiwa salama haingii akilini
kwamba ni wapiganaji wenye mafunzo ya kawaida.
“Wakati
risasi zinapigwa na serikali inatuambia tuchukue tahadhari kwa mtu
tusiyemjua tumtolee taarifa tuliamini lazima watakamatwa hata kama si
wote. Lakini tulipoambia hali imetulia lakini hajakamatwa hata mmoja
tulishangaa sana,” alisema mkazi huyo akiomba asitaje jina lake.
Akizungumza
na Uwazi, mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Amboni aliyejitambulisha kwa
jina moja la Hassan alisema magaidi hao walipiga kambi kwenye mapango
hayo tangu mwaka 2013.
“Sisi
tulianza kuwaona mwaka 2013, sikumbuki mwezi. Lakini walionekana kama
wachimba kokoto ndiyo maana walidumu kwa muda wote huo. Pale kuna sehemu
watu wanachimba kokoto.”
ILIKUWA KAMA KWAO
“Naweza
kusema walipatawala pale kwani ilikuwa kukicha, wengine walikuwa
wakienda mjini wengine wanashinda palepale. Haikuwa rahisi kudhani ni
magaidi,” alisema Hassan.
MAMBO MATATU YAIBUKA
Hata
hivyo, wananchi hao ambao wanasema mpaka sasa hawana amani licha ya
kuwepo kwa askari polisi kila kona kulinda, walisema kuna mambo matano
ambayo polisi wamekaa kimya kuyatolea ufafanuzi.
Polisi wakiwa kwenye mapambano.
MOSI
“Sisi
wakazi wa hapa palipotokea mapigano tunajiuliza, kwa nini polisi
wameshindwa kutuambia ukweli wale ni akina nani badala ya kusema
majambazi.
“Tangu lini majambazi wanapiga kambi mahali? Mimi ninavyojua, majambazi
hufanya uhalifu na kurudi makwao. Tena naamini majambazi tunapanga nao
nyumba tunazoishi au tunaishi nao mtaa mmoja au jirani,” alisema Almasi,
mkazi wa Kijiji cha Kilomoni.
PILI
Wakazi
hao walikwenda mbele zaidi na kusema kuwa, tangu Tanzania ipate uhuru
haikuwahi kutokea majambazi wakapambana na polisi halafu polisi
wakashindwa hadi kuita wanajeshi na wasikamatwe hata mmoja?
TATU
Wakazi
hao waliendelea kudai kuwa, wamesikia tetesi zinazodai mwanajeshi
aliyeuawa yalitokea makosa ya kiufundi kutoka kwa majeshi yetu lakini
wanashangaa kimya cha polisi licha ya habari hizo kusambaa sana Amboni.
“Sisi tunasikia yule askari aliyeuawa ilitokana na makosa ya kiufundi
kutoka kwa wenzake. Watu wengi hapa Mafuriko wanasema wamesikia hivyo,
jeshi lingekanusha au kufafanua kama kuna ukweli,” alisema Mgaya, mkazi
wa kijiji hicho.
WANANCHI MAPEMA NDANI
Baadhi
ya wakazi walizungumza na Uwazi walisema licha ya kuwepo kwa polisi
maeneo hayo lakini wanalazimika kuingia ndani mapema kwani kuna
minong’ono kuwa, wahalifu hao wamejipanga kurudi na nguvu mpya baada ya
kwenda kukutana na wenzao kwenye nchi jirani lakini jeshi la polisi
mkoani hapa limekanusha uvumi huo na kuwataka wananchi waendelee na
shunguli zao za kila siku.
Magaidi wa Al-Shabaab.
AL- SHABAAB ALIYEKIMBILIA KANISANI DAR...
Wakati
huohuo, kijana mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Shaban, mwenyeji wa
Iringa ambaye alikiri kanisani kupewa mafunzo ya kigaidi nchini
Afghanistan ili kwenda kutumika na Kundi la Al-Shabaab nchini Somalia
ametoweka.
Akizungumza na Uwazi, Mchungaji wa Kanisa la Victoria lililopo
External-Ubungo jijini Dar, John Said alisema Shaban alifika kanisani
kwake mwaka jana na kutoa ushuhuda mzito kwamba yeye na Watanzania
wenzake wawili walipelekwa Afghanistan kwa ajili ya mafunzo ya dini
lakini walipofika wakakuta ni mafunzo ya kigaidi.
“Shaban
alitoweka, haji tena kanisani kama zamani. Alipokuja kwa mara ya kwanza
alitoa ushuhuda huo mzito lakini baadaye akakata mguu,” alisema
mchungaji huyo.
Katika
ushuhuda wake, Shaban alisema kuwa, baada ya kufuzu walipelekwa Somalia
kuungana na Al-Shabaab na kupigana na majeshi ya serikali ya nchi hiyo
kwa kutumia silaha nzito lakini mwishowe aliamua kutoroka kurudi nchini.
Anasema:
“Siku moja katika mapambano na majeshi ya serikali nilishuhudia wale
wenzangu wawili wakiuawa kwa risasi, mimi nikatoroka katika eneo la
mapigano kwa kuruka ukuta, ndiyo nikarudi hapa nyumbani Tanzania.”
UWAZI LAZUNGUMZA NA CHAGONJA
Baaada
ya gazeti hili kuchimba yote hayo, lilimtafuta Kamishna wa Oparesheni
ya Mafunzo Jeshi la Polisi Tanzania, Paul Chagonja ambapo alipopatikana
na kumsimulia mambo yote mpaka ya Shaban, alisema:
“Mimi niko nje ya nchi kwa kazi ya kitaifa, wasiliana na Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Tanga (Juma Ndaki) akupe maendeleo ya oparesheni yetu
kule.
“Kuhusu huyo Shaban, nawasiliana na kitengo cha intelejensia sasa hivi
ili atafutwe mpaka apatikane. Si yeye tu msako mkali unaendelea kwa
umakini juu ya watu hao.”Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga alipotafutwa
juzi, simu yake ilikuwa hewani lakini hali ya hewa ilikuwa mbaya hivyo
kukosa usikivu.