
Mbeya.
Wakizungumza na waandishi wa habari wilayani hapo, wafugaji hao,
walidai kuwa imekuwa kawaida kwa askari hao kukamata mifugo na kuwatoza
faini kubwa na wakati mwingine kuwashambulia kwa vipigo.
Mmoja wa wafugaji hao, Igembe Mahola, Mkazi wa Kijiji cha Iyala,
alidai hivi karibuni ng’ombe wake 143 walikamatwa na askari hao wa
wanyamapori wakidaiwa kukutwa ndani ya hifadhi na alipofuatilia,
alishushiwa kipigo kisha kutozwa faini ya Sh. milioni 9.
Mahola alidai kuwa kwenye stakabadhi yake, aliandikiwa kuwa amelipa
faini ya Sh. milioni 5 badala ya Sh. milioni 9 alizoamriwa kulipa na
askari hao.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Wilaya ya Mbarali,
Makeresia Pawa, alisema askari hao wanatumia udhaifu wa serikali juu ya
migogoro ya mipaka iliyopo kujinufaisha.
Pawa alisema mara kadhaa imeripotiwa na wafugaji kuwa askari hao
huswaga ng’ombe ndani ya hifadhi baada ya kuwakuta wakiwa katika maeneo
ya jirani ili kujipatia fedha.
“Tumepaza sana sauti zetu sisi wafugaji na inaonekana serikali
imekuwa ngumu kutuelewa katika hili hivyo basi tunaiomba kutusikiliza
kilio hiki vinginevyo tutakuja na maazimio magumu sana, ”alisema Pawa.
Akijibu malalamiko hayo, Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha, Christopher
Timbuka, alisema hajayapata ila anachofahamu askari hao kuendelea
kutekeleza wajibu wao ili kuhakikisha hakuna mifugo inayoingia ndani ya
hifadhi hiyo ili kutunza mazingira.
Timbuka alisema madai ya kutozwa faini kubwa na kupewa stakabadhi
zenye viwango pungufu, amekuwa akiyasikia, lakini wafugaji wameshindwa
kutoa ushirikiano kwa kuwataja majina askari wanaojihusisha na vitendo
hivyo ili hatua zichukuliwe.
Ametoa wito kwa wafugaji hao waache kupeleka mifugo yao ndani ya
hifadhi hiyo ili kuepukana na adha hizo wanazokutana nazo baada ya
kukamatwa.
CHANZO:
NIPASHE