FUNGA KAZI LOWASSA,DK.MAGUFULI HII HAPA.

By | 23:48


Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Wakati ikiwa imebaki siku moja tu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu keshokutwa, kambi za wagombea urais wanaochuana vikali kutokana na wingi wa watu wanaojitokeza kwenye mikutano yao, Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), zimeweka wazi baadhi ya mikakati yao ya kufunga kazi na kujihakikishia ushindi wa kishindo.
 
Taarifa zilizotolewa na wasemaji wa kambi zote mbili jana zilidhihirisha kuwa, mikakati hiyo ya saa 48 zilizobaki kuanzia leo, ndiyo karata ya mwisho ya kila upande kujikubalisha kwa wapigakura ili mwishowe wagombea wao wavune kura nyingi na kuingia Ikulu kumrithi Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake baada ya kumalizika kwa uchaguzi.
 
Mbali ya Magufuli na Lowassa ambaye pia anaungwa mkono na muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chama cha Wananchi (CUF), NCCR- Mageuzi na NLD, wagombea wengine wa urais ni Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo, Janken Kasambala wa NRA, Hashim Rungwe wa Chaumma, Fahmy Dovutwa wa UPDP, Chifu Lutasola Yemba wa ADC na Maximillian Lymo wa TLP.
 
MAGUFULI, JK, SAMIA KUMALIZIA MWANZA
Mjumbe na Msemaji wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba, aliwambia waandhishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa, wataanza ratiba ya kihistoria ya kuhitimisha kampeni zao kuanzia leo Jangwani, jinini Dar es Salaam na mgombea wao, Magufuli na mgombea mwenza, Samia Suluhu watafunga kazi jijini Mwanza Jumamosi ijayo, huku wakiwa jukwaa moja na Rais Jakaya Kikwete.
 
Makamba alisema mbali na ufungaji huo utakaofanyika Jumamosi, pia makada wao kadhaa ‘wazito’ watasambazwa katika mikoa saba nchini kote kuhakikisha wanavuna kura nyingi kadri iwezekanavyo. Mbali na Mwanza na Dar es Salaam, Makamba aliitaja mikoa mingine kuwa ni Tanga, Mbeya, Mtwara, Kigomba, Kilimanjaro na Mara.
 
Alisema katika mkoa wa Tanga, Katibu Mkuu wa chama chao, Abdulrahman Kinana, ndiye atakayeongoza makada wengine kushambulia eneo hilo kwa kutoa sera na ahadi zinazotekelezeka, huku kazi kama hiyo ikifanywa pia na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa atakayekuwa jijini Mbeya.
 
Makamba alieleza zaidi kuwa katika mkoa wa Mtwara, kampeni zao zitafungwa na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na mkoani Kigoma atakuwapo Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula.
 
Alisema katika mkoa wa Kilimanjaro, Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuph Makamba ndiye atakayeongoza kampeni hizo, huku Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Joseph Warioba, akiongoza kazi ya kufunga kampeni zao mkoani Mara.
 
“Mikutano hii ya ufungaji wa kampeni itakuwa mikubwa na itarushwa moja kwa moja kupitia vituo vya luninga vitano na radio mbalimbali 67 nchini kote,” alisema Makamba.
 
Alisema mikutano hiyo pia itaunganishwa moja kwa moja na hotuba ya mgombea urais, Dk. Magufuli kutokea mkoani Mwanza kupitia TV zitakazofungwa kwenye mikutano yote hiyo.
 
“Kwanza tunatarajia kuongeza maeneo mengine ya kufunga mikutano kati ya leo na kesho, lakini pia hotuba ya Dk. Magufuli itakuwa live (itarushwa moja kwa moja) na watu wote walioko kwenye mikutano watafuatilia kupitia TV kubwa zitakavyokuwa zimefungwa uwanjani,” alisema makamba na kuongeza kuwa mikutano hiyo inatarajiwa kuanza kurushwa moja kwa moja kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 12:00 jioni.
 
Nipashe imebaini vilevile kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, Bernard Membe, ataongoza harakati za kufunga kampeni hizo mkoani Lindi katika Jimbo la Ruangwa.
 
Membe ambaye pia alikuwa miongoni mwa makada waliofika hatua ya tano bora katika mbio za urais ndani ya chama hicho, atamuombea kura Magufuli na pia wagombea ubunge na madiwani.
 
DAR KUMALIZA KAMPENI LEO
Makamba alisema katika ratiba yao hiyo ya kufunga kazi, Magufuli atamaliza kampeni zake jijini Dar es Salaam leo, kwenye viwanja vya Jangwani ambako ndiyo walikoanzia kampeni zao Agosti 22, mwaka huu.
 
“Kwa sababu tumejikita kufungia kampeni mikoani, jijini hapa tutafunga kampeni zetu kesho (leo) kuanzia saa 9:00 alasiri,” alisema Makamba.
 
Kadhalika, Makamba alisema kuwa licha ya kampeni zao za urais kwa jiji la Dar es Salaam kuhitimishwa leo, bado wagombea wao wa ubunge na udiwani wataendelea na kampeni zao kumalizia kazi na kwamba, watakuwa wakiongozwa na wagombea wao wa ubunge mkoani humo.
 
MATUMAINI YA USHINDI CCM
Katika hatua nyingine, Makamba alisema chama chao (CCM) kinatarajia kuibuka na ushindi wa asilimia 69 na kwamba ni matumaini yao vilevile kuwa uchaguzi utafanyika kwa amani na utulivu.
Alisema imani yao ya ushindi inatokana na matokeo ya tafiti zilizofanywa na taasisi mbalimbali na pia tathmini zao ndani ya chama.
 
“Chama tunaridhika na ubora wa kampeni tulizofanya, licha ya kuwapo kwa changamoto za hapa na pale… Dk. Magufuli na Samia Suluhu Hassan wamefanya kazi kubwa inayotuhakikishia ushindi usiyopungua asilimia 69,” alisema Makamba.
 
Akizungumzia hoja ya kulinda kura umbali wa mita 200 kutoka vituo vya kupigia kura inayotolewa na viongozi wa Ukawa, Makamba alisema mawakala wa vyama waliowekwa vituoni wanatosha kufanya kazi hiyo.
 
Alisema ili kudhibiti wafanya fujo, CCM itatoa namba maalum ya kutuma ujumbe mfupi wa maneno au kupiga simu pale Watanzania watakapobaini vitendo vya kuvuruga amani na taratibu za uchaguzi kama kuzuia watu kufika katika vituo vya kura.
 
Aidha, Makamba alisema wanataraia kupata matokeo kutoka kwa mawakala wao watakaowaweka vituoni na pia mtandao maalum wa chama (CCM) utakaowawezesha kujua mwenendo wa ushindi wao kufikia saa 4:00 usiku.
 
FUNGA KAZI YA UKAWA
 ‘Makombora’ ya Ukawa katika kuhitimisha kampeni zao yataanza leo wakati mgombea urais, Lowassa atakapolihutubia taifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari vikiwamo vituo vya luninga, radio na mitandao ya kijamii kama twitter na facebook.
 
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, alisema Lowassa atahutubia leo (Ijumaa) kuanzia saa 3:00 usiku.
 
“Kupitia hotuba hiyo kwa taifa, Lowassa atazungumza na Watanzania wote, ndani na nje ya nchi na watu wa mataifa yote kuhusu Tanzania mpya itakayotokana na mabadiliko makubwa ya kimfumo, kiutawala na utendaji wa serikali atakayoiunda baada ya Watanzania kumpatia dhamana ya kuwa mkuu wa nchi, Amiri Jeshi Mkuu na kiongozi mkuu wa serikali hapo Oktoba 25, 2015,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.
 
Aidha, taarifa hiyo inaeleza kuwa Lowassa atatumia muda huo kuwashukuru Watanzania wote kwa namna walivyomuunga mkono kwa upendo mkubwa yeye, mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji na Ukawa kwa ujumla kuelekea hatua ya kuleta mabadiliko ya kuhitimisha utawala wa nusu karne wa CCM, lengo likiwa ni kuwa na serikali itakayotokana na watu kwa ajili ya watu ambao ni umma wa Watanzania.
 
KUFUNGA KAZI DAR, MWANZA
Akieleza kuhusu ufungaji wao wa kampeni, Makene aliiambia Nipashe kuwa, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ataongoza kazi hiyo jijini Mwanza, kwenye Jimbo la Nyamagana linalotetewa na mgombea anayewakilisha Ukawa, Ezekiel Wenje.
 
Kadhalika, Makene alisema katika majimbo na kanda 10 za chama hicho, wataendelea kufunga kampeni kwa kuwatumia wagombea ubunge wa maeneo husika na pia baadhi ya viongozi wao wa juu.
 
Alizitaja kanda hizo kuwa Magharibi, Kati, Pemba, Unguja, Pwani, Kaskazini, Victoria, Serengeti, Nyasa na Kusini.
Makene aliongeza kuwa, watafunga kampeni zao kitaifa jijini Dar es Salaam, kwenye viwanja vya Jangwani Jumamosi, ambako Lowassa na viongozi kadhaa wa kitaifa wa Ukawa watahudhuria.
 
Alisema mkutano huo utafanyika kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 9:00 alasiri na utarushwa moja kwa moja na vituo vya luninga vya ITV, Channel Ten, Clouds, na radio za East Africa na Radio One.
 
“Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salimu Mwalimu, atamalizia kampeni zake visiwani Zanzibar,” alisema Makene.
“Mambo mengine ya kimkakati kwa ajili ya ushindi ni ya ndani yetu (Ukawa),” alisema.
 
*Imeandikwa na Mary Geofrey, Salome Kitomari  na Abdul Mitumba, 
 
CHANZO: NIPASHE
Newer Post Older Post Home