PINDA :SIJAHAMA CCM NA SITAHAMA.

By | 02:15


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema hajahama Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na baadhi ya watu na mitandao ya kijamii kwamba amejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
 
Pinda alitoa kauli hiyo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti juzi na wakazi wa Majimbo ya Mpanda Mjini na Kavuu kwenye mikutano minne ya hadhara iliyofanyika katika kata za Kakese, Kibaoni, Usevya na Majimoto wakati akifunga kampeni za uchaguzi mkoani Katavi.
 
“Kuna picha zimesambaa mitandaoni zinadai nimehamia Chadema. Hivi kweli sasa hivi nahamia huko ili iwe nini?” Alihoji.
 
Alisema picha wanazozisambaza ni za mwaka 2012 ambazo zilipigwa wakati akionyesha kwa wananchi moja ya kadi alizopokea kutoka kwa wanachama wa Chadema. Katika moja ya picha hizo, Waziri Mkuu Pinda anaonekana akiwa na mlinzi wake huku akionyesha kadi ya Chadema.
 
Hata hivyo, hakuna kiongozi yeyote wa Chadema anayeonekana akimkabidhi kadi kama mwanachama mpya.
 
CHANZO: NIPASHE
Newer Post Older Post Home