
Hali hiyo hukwamisha maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosseah (pichani), wakati akifungua jengo jipya la taasisi hiyo mkoani Mbeya juzi.
Dk. Hosseah alisema kutokana na upotevu huo, Taifa limekuwa likikosa fedha nyingi ambazo kama zingetumika kwa uadilifu, zingewaletea wananchi maendeleo makubwa.
“Kila mwaka taifa letu linapoteza asilimia 30 ya Pato la Taifa, sasa jaribu kufikiria kama hiki kiasi cha asilimia 30 kingerudi katika maendeleo, nadhani tungeona taifa letu linastawi kwa kasi kubwa,” alisema Dk. Hosseah.
Akizungumzia mafanikio ya taasisi hiyo, Dk. Hosseah alisema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Takukuru ilifanikiwa kuchunguza na kushinda kesi kubwa za rushwa 1,993.
Alisema katika uchunguzi huo, Takukuru iliokoa zaidi Sh. bilioni 88 na kuzirejesha serikalini, kiasi ambacho alisemaa ni kama kisingeokolewa kingeishia mifukoni mwa wala rushwa.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, alisema ili vita dhidi ya rushwa ifanikiwe, ni lazima kila mtu aichukie kwa kutambua madhara yake.
Alisema baadhi ya viongozi wa umma wanashiriki katika vitendo vya rushwa bila kujua madhara yake na hivyo wanahitaji elimu ya kutosha ili waichukie na kujiweka mbali na vitendo hivyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mbeya, Xavery Mhela, alisema changamoto inayoikabili Takukuru katika vita dhidi ya rushwa, ni pamoja na baadhi ya mashahidi kukosa ujasiri wa kutoa ushahidi mahakamani. Alisema hali hii husababisha hata viongozi wanatuhumiwa kwa rushwa kuendelea kukalia ofisi za umma, hali ambayo inasababisha mapambano dhidi ya rushwa kuwa magumu.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge walio katika Mapambano ya Rushwa barani Afrika (Apnac), tawi la Tanzania, Dk. Mary Mwanjelwa, alisema vita dhidi ya rushwa ni kubwa lakini watu wasikate tamaa kukabiliana nayo.
CHANZO: NIPASHE