SERIKALI YAKIRI UMEME HALI MBAYA.

By | 23:41

Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.
Hatimaye serikali imekiri kuwapo kwa hali mbaya ya upatikanaji wa umeme nchini kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo ya kukosekana kwa maji ya kutosha ya kuzalisha nishati hiyo katika mabwawa sita yaliyopo nchini.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, ndiye aliyeeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, ikiwa ni siku moja tu baada ya gazeti hili kueleza kwa kina taarifa iliyotolewa na Shirika la Umeme Tanzania  (Tanesco) ukweli huo katika kipindi hiki ambacho taifa lingali likikabiliwa na mgawo usio rasmi wa umeme.
Simbachawene alisema uzalishaji wa umeme utokanao na chanzo cha maji umeporomoka kwa takriban asilimia 85 baada ya mabwawa kukosa maji ya kutosha, huku Bwawa la Mtera likishindwa kuzalisha kabisa.
Kwa kawaida, umeme unaozalishwa katika mabwawa sita ya Mtera, Kidatu, Hale, Nyumba ya Mungu, Kihansi na Maporomoko ya Pangani huwa ni megawati 561. Hata hivyo, kiwango cha jumla kinachozalishwa sasa na mabwawa hayo ni megawati 105 tu, sawa na asilimia 18.7 ya uwezo wake. 
“Umeme wa maji umeondoka ghafla kwa kiasi cha takriban asilimia 85... kwakweli umeme wa maji unakaribia kutoweka na hili lazima lilete shida. Lakini serikali inaendelea na jitihada za kutatua tatizo hili kupitia umeme wa gesi,” alisema Simbachawene.
Hata hivyo, alisema hata kama kuna umeme utokanao na vyanzo vingine kama gesi asilia, bado umeme utokanao na maji unahitajika kwa kiasi kikubwa ili kuondoa tishio la nchi kuwa gizani.
Alieleza miongoni mwa sababu za kukauka kwa mabwawa ya kuzalishia umeme ni shughuli za kibinadamu kufanyika kwenye vyanzo muhimu vya maji yanayoingia (kwenye mabwawa), ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa mashamba makubwa ya mpunga na mazao mengine.
“Maji yanapotelea kule kwenye mashamba ya mpunga kama Kapunga na mengine. Hili siwezi kuliongelea peke yangu, lakini lazima tukae kama serikali tuangalie namna ya kujikwamua kwa kuchukua maamuzi... hakuna namna nyingine. Hata kama tuna umeme wa gesi, lakini lazima na wa maji uwepo,” alisema Simbachawene.
Katika hatua nyingine, Simbachawene alisema wanatarajia kuzima kabisa mitambo ya Bwawa la Mtera kwa sababu maji yamefikia kiwango cha mwisho cha chini. Hivi sasa, Mtera linalotegemewa kuzalisha megawati 80, halizalishi kabisa kutokana na ukame wa maji uliolikumba.
“Haijawahi kutokea, lakini safari hii Mtera tutazima maana hakuna maji kabisa. Tumefika mwisho kabisa... hatuwezi
kuendesha mitambo wakati maji hakuna,” alisema Simbachawene, kabla ya kuongeza kuwa hali ingekuwa mbaya zaidi kama kusingekuwapo uzalishaji wa umeme utokao katika vyanzo vingine kama gesi.
Alisema mahitaji halisi ya umeme nchini ni kuanzia megawati 870 na zaidi, hivyo ni wazi kuwa kuwapo kwa megawati 105 pekee za maji kwa sasa kunasababisha pengo kubwa la mahitaji halisi.
Bwawa la Kidatu lenye uwezo wa juu wa kuzalisha megawati 204, hivi sasa linazalisha megawati 27 (asilimia 13.2); Kihansi lenye uwezo wa juu wa kuzalisha megawati 180, uzalishaji wake hivi sasa umeshuka hadi megawati 51.5 (asilimia 28.6); Nyumba ya Mungu lenye uwezo wa juu wa kuzalisha megawati 8, linazalisha megawati 5.5 tu (asilimia 68.8) ya uwezo wake wa juu; Hale lenye uwezo wa kuzalisha megawati 21 hivi sasa linazalisha megawati 4 (asilimia 19) na maporomoko ya maji ya Pangani (New Pangani Falls) yenye uwezo wa kuzalisha megawati 68, yameathiriwa na kupungua kwa kiwango cha maji hadi kuzalisha Megawati 17 tu (asilimia 25).
UMEME WA GESI, MAFUTA
Simbachawene alisema serikali inatarajia upatikanaji wa gesi inayotoka Mtwara utafidia upungufu uliopo na kwamba hivi sasa tangu mitambo ya gesi iwashwe, imefikia uwezo wa kuzalisha megawati 135.
Kuhusiana na umeme utokanao na mafuta, alisema huo ni ghali mno kwa sasa kutokana na hali ya uchumi kwani fedha nyingi zimeelekezwa katika uchaguzi na kwamba, kiwango kinachozalishwa ni megawati 110 tu.
Alisema kwa siku moja, kiasi cha Sh. bilioni 3 hadi 5 hutumika kwa ajili ya umeme wa mafuta na hivyo wananchi wanapaswa kuvumilia wakati jitihada za kuongeza umeme utokanao na gesi zikiendelea kufanyika kwani huo ndiyo wenye gharama nafuu kuliko wa mafuta.
“Kwa sasa niwahakikishie jitihada zinafanyika za Shirika la Umeme Tanesco na TPDC  kuhakikisha ndani ya wiki hii inawashwa mitambo ya Kinyerezi I, na hapo wanategemea kupata megawati 75 ingawa kiufundi watu waliowauzia mitambo wamesema wataanza na megawati 70," alisema.
CHANZO: NIPASHE
Newer Post Older Post Home