
Akizungumza na Wahariri alipotembelea ofisi za Kampuni ya The Guardian Ltd jana, Rodriguez alisema wanaufuatilia kwa karibu uchaguzi mkuu kwani wangependa Tanzania ipate viongozi wa kushughulikia changamoto zinazokabili taifa hili.
“Ninasema wazi Tanzania imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuandaa uchaguzi huru na wa haki,” alisema Rodriguez na kuongeza kuwa Tanzania ilikuwa tofauti na majirani zake.
Rodriguez alisema Tanzania ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine na hasa zinazoizunguka kwani hawajasikia mizengwe ya kubadilisha katiba au viongozi kuvunja katiba kwa kujiongezea vipindi vya uongozi.
Hata hivyo, alisema kumekuwa na changamoto kadhaa zinazojitokeza, lakini zimekuwa zikishughulikiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na vyombo vya dola.
“Siyo kwamba hakuna matatizo, lakini pale yanapojitokeza yamekuwa yakishughulikiwa vizuri. Hili ni jambo zuri linaloifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano,” alisema Rodriguez. Alisema UN inafahamu kuwa uchaguzi huu ni muhimu ikizingatiwa kuwa vijana watajitokeza kwa wingi kupiga kura kutokana na changamoto nyingi zinazowafanya kupigania mabadiliko kwenye maisha yao.
Alisema ushahidi wa jambo hilo ni jinsi vijana wanavyojitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni za wanaowania urais, ubunge na udiwani katika sehemu mbalimbali nchini.
“Kutakuwa na wapiga kura vijana wengi na idadi yao kubwa watakuwa wanapiga kwa mara ya kwanza ukikumbuka kuwa wana changamoto nyingi za kimaisha,” alisema Rodriguez.
Alizitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili vijana kwenye uchaguzi huu kuwa ni tatizo la ajira na wengine kupewa nafasi ambazo ziko chini ya kiwango cha elimu zao.
“Vijana wengi wa Tanzania wanakabiliwa na tatizo la ajira na hata wengine kukosa fursa, lakini pia kuna kundi lililoelimika ila limekuwa likilazimika kufanya kazi ambazo ziko chini ya kiwango cha elimu yao,” alifafanua Rodriguez, ambaye aliwahi kuwa Mwakilishi wa UN nchini Afghanistan.
Vijana wanakadiriwa kufikia asilimia 61 ya idadi ya watu wote Tanzania, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali.
Rodriguez alisema kuwa UN wanaufuatilia kwa makini uchaguzi huu, lakini kuna kitu ambacho kimemsikitisha wagombea wamekuwa wakimwaga ahadi nyingi bila kuzitolea ufafanuzi wa utekelezaji wake.
“Nawafuatilia wagombea na nimekuwa nikisoma wakiahidi mambo mengi, lakini bila ya kutoa uchambuzi wa kina wa jinsi watakavyotekeleza ahadi zao. Nadhani kasoro ndiyo naiona hapo,” alifafanua Rodriguez.
Alisema pia angependa kusikia wagombea wakizungumzia Mpango wa Maendeleo Endelevu wa Umoja wa Mataifa (SDG).
Alisema SDG utakuwa na umuhimu mkubwa wakati serikali ijayo itakapokuwa inatekeleza mipango yake ya maendeleo.
“Tutashirikiana na serikali ijayo katika kutekeleza mpango wa SDG na ndiyo maana tunafuatilia uchaguzi huu.
Tunataka kuona mpango huu ukiingizwa katika mipango ya utekelezaji wa maendeleo ya nchi,” aliongeza Rodriguez.
Alisema mpango huo wa UN unahimiza suala la kushirikiana na serikali zilizochaguliwa kidemokrasia.
“Tumeshuhudia wenyewe jinsi mnavyoendesha uchaguzi wenu kidemokrasia. Ina maana mtakuwa miongoni mwa nchi za mfano katika utekelezaji wa mpango wa SDG,” alifafanua.
Rodriguez alisema mpango wa SDG wenye malengo 169, ulipitishwa hivi karibuni wakati wa kikao cha Baraza Kuu la UN hivi karibuni.
Alisema angependa kuona wagombea wa nafasi mbalimbali za uchaguzi wakizungumzia mpango wa SDG na jinsi watakavyoingiza kwenye utekelezaji wa sera zao.
Rodriguez alisema ajenda ya SDG inalenga katika kumaliza umaskini, kwa hiyo itakuwa jambo la ajabu ikiwa haitaingizwa kwenye ajenda za maendeleo ya taifa.
Mwakilishi huyo wa UN alisema Tanzania itaathimisha miaka ya 70 ya kuanzishwa kwa UN Oktoba 13, mwaka huu.
Alisema kuwa ajenda kuu ya sherehe hizo ni suala la tabianchi ambalo limekuwa likitawala katika medani ya siasa nchini.
Hata hivyo, alisema ameshangazwa kuwa suala la tabianchi halimo kwenye ajenda za wanasiasa nchini.
“Nashangaa kuona wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi hawazungumzii tatizo la tabianchi wakati linagusa watu wengi,” aliongeza.
CHANZO: NIPASHE