TUONGEE WAZAZI:TUMIA KOSA LA MTOTO KUMJENGEA NIDHAMU.

By | 22:15





Jamii zetu za Kiafrika zilikuwa na taratibu nzuri za kumwadhibu mtoto kwa lengo la kumfundisha pindi anapokosea. Taratibu hizi zililenga kumpa mtoto uzoefu kwa kumjenga kukabiliana na changamoto za maisha yaliyomzunguka.
Viboko na nguvu wanayotumia wazazi wa leo haikuwa kati ya njia walizotumia wazee wetu katika kujenga tabia za watoto wao. Wazazi/walezi wa leo hutumia njia ya fimbo au kipigo cha aina yoyote ili kumkanya au kumkomesha mtoto asirudie tena. Leo tutaangalia madhara ya kumpiga mtoto ili awe na adabu na kama zipo namna tunaweza kutimiza majukumu yetu ya kuhakikisha mtoto anakuwa na tabia njema bila kutumia nguvu.
Mtaalamu na mwandishi mahiri katika saikolojia ya makuzi ya mtoto Sarah Kovac anasisitiza kuwa kumpiga mtoto mfano kwa fimbo, vibao, ngumi, mateke na kadhalika kwa malengo ya kumfundisha mtoto asirudie kosa humuumiza mtoto kimwili, kisaikolojia, na mara nyingi humfanya mtoto kutokujiamini na hata kupunguza ukaribu na mlezi/mzazi bila kupata mafunzo yoyote au kuelewa chochote kwenye kosa husika.
Uzoefu unaonyesha kwamba kumuumiza mtoto kwa lengo la kumkomesha hakumjengi kujirekebisha kitabia bali mara nyingi humfanya kuigiza tabia njema kwa muda tu na kuficha makucha ya tabia mbaya.
Vilevile humfanya mtoto asiweze kujisimamia mwenyewe kutenda mema mpaka atishiwe adhabu ama kipigo. Yaani ukitaka kumtuma mwanao kijiko kwa mfano, lazima useme, ‘usipoleta kijiko nitakuchapa.’
Wataalamu wa makuzi wanakubaliana na taratibu tulizozitupa za mababu zetu zilizolenga kutoa adhabu stahiki ili kumfunza mtoto aweze kudhibiti tabia yake, kung’amua kati ya jema na baya mwenyewe na kufanya jambo si kwa kuogopa adhabu bali kwa kujua kuwa ni jambo sahihi kufanya. “Unavyoongeza kuwapiga watoto (kila wanapokosea), wanazidi kupoteza uwezo wa kujisimamia wenyewe. Mara nyingi wanazoea kusimamiwa na wazazi, walezi n.k. lakini je, kama hamna anaewaangalia na kuwasimamia, utegemee nini?” Anauliza Sarah Kovac.
Aina ya adhabu unayoitumia kumkanya mtoto siku zote imjengee uwezo wa kuwa na nidhamu popote pale alipo, uwepo -usiwepo. Ifike mahala mtoto asidanganye siyo kwa kuwa atachapwa akidanganya ila kwa kuwa anaelewa kusema uongo siyo jambo jema.
Tumia fursa hii kujenga uwezo wa mtoto kutatua matatizo yake na ya watu wanaomzunguka. Fursa ya aina hii inaondoa uwepo wa nidhamu ya uoga na atafanya mambo bila kuwa na wasiwasi wa kupigwa, kufokewa au kudhalilishwa kwa namna yoyote. Watoto wa aina hii huwa na uwezo mkubwa wa kudadisi na kujifunza mambo mapya kwa uhakika wa kurekebishwa kwa upendo na kuonyeshwa njia sahihi ya kufanya mambo pale anapokosea. Malezi ya namna hii humpa mtoto moyo wa uthubutu katika maisha.
Mfano, ikitokea ameharibu labda kifaa cha umeme, usighadhibike kupita kiasi bali tumia fursa hii kumuelewesha asiharibu tena. Muelezee namna ya kutumia kifaa hicho kwa ufasaha, manufaa yake na gharama za kununua kingine au kukitengeneza. Hii itumike kwa mtoto anayeelewa (mkubwa kiumri kuanzia miaka mitatu na kuendelea).
Kwa mtoto asiyeelewa (mdogo), weka vifaa kama hivi mbali naye. Njia hii humfanya mtoto kutokuviogopa vifaa hivi na kuvizoea na humuongezea udadisi. Huwezijua, pengine siku moja mtoto wako atakuja kuwa mhandisi mzuri wa kutegemewa na taifa kwa kuwa haukuua udadisi wake akiwa mdogo.
Makala haya yameandaliwa na wataalamu wa makuzi toka C-Sema .
MWANANCHI.

Newer Post Older Post Home