UPIGAJI KURA KIMARA WAINGIA DOSARI.

By | 23:23




Wapiga kura wakihakiki majina yao
Wapiga kura wakihakiki majina yao 

By Joyce Mmasi, Mwananchi
Dar es Salaam. Shughuli za upigaji kura katika kituo cha EDP kilichoko eneo la Kimara Stop Over jana zilisimama kwa muda na wapigakura kufungiwa ndani ya kituo baada ya kukosekana kwa karatasi za kupigia kura za mgombea urais.
Msimamizi msaidizi wa kituo hicho, Jastina Khatibu alikiri kuwapo kwa changamoto hiyo akisema badala yake, wapigakura hao walitakiwa kupiga kura ya ubunge na udiwani.
Alisema wapigakura hao, walilazimika kusubiri kwa muda ili kupiga kura ya urais.
Kituo cha EDP kina vituo vidogo vinane vyenye wastani wa wapiga kura 450.
Hadi jana saa 4:00 asubuhi kilikuwa bado hakijafunguliwa kuanza kazi.
Msimamizi mkuu wa kituo hicho Julias Nyamhonga alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliwasilisha vifaa pungufu tofauti na matarajio yao.
Katika kituo cha Temboni, wananchi zaidi ya 400 wenye majina yanayoanzia na herufi P walikwama kupiga kura kwa madai kile walichosema majina yao yapo kituo kingine umbali wa zaidi ya kilometa mbili.
Hata hivyo kulitokea sintofahamu baada ya majina ya wananchi hao kukosekana kwa mara nyingine katika kituo walichokwenda kuyaangalia.
Hata hivyo, hawakupatiwa msaada na kukosa haki ya kupiga kura licha ya kuwa na vitambulisho.
Msimamizi wa Kituo cha Temboni, Albert Feni alisema kati ya vituo 18 vilivyokuwa vimetengwa kwa ajili ya upigaji kura ni vituo 10 pekee vilivyokuwapo.
Katika Kituo cha Shule ya Msingi Saranga wananchi walianza kupigia kura saa 8.12 mchana kutokana na kushindwa kuwatambua wapigakura baada ya kukosa daftari lenye orodha ya majina yote.
Msimamizi wa kituo hicho, Rukia Aziz alisema daftari hilo lilipotea hivyo kuwalazimu kwenda kufuata lingine (NEC).

Newer Post Older Post Home